Wednesday, June 11, 2014

Mjue Roho Mtakatifu - 1 : Watu Husema Roho ni Nani?

Pengine umeshawahi kusikia maneno kama “Roho ameniambia” au “Sijisikii Roho akiniruhusu” na yanayofanana na hayo. Au hata umewahi kuona “mlokole” akifanya vituko kwa madai kuwa “Roho ameniambia”. Huyu Roho yukoje? Umewahi pia kujiuliza kwa nini pamoja na kwamba Roho ni mmoja lakini watu haohao wanaoongozwa na Roho wanapingana? Ukweli ni upi?

Katika makala hii nitakuletea mfululizo wa Neno la Mungu linasema nini juu ya Roho Mtakatifu. Kabla hatujaona Biblia inasema nini juu ya Mtu muhimu kabisa huyu, hebu tuangalie lile swali maarufu la Yesu “watu hunisema kuwa mimi ni nani?”. Je watu Husema Roho Mtakatifu ni nani?

Waislamu wanasema ni Malaika Jibril

Unaweza kuwa umeshtuka, lakini ukweli ni kuwa Koran inamtaja Roho Mtakatifu. Surat Al-Baqara ayat 87 (2:87) Koran inasema (msisitizo ni wangu)

“Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukafuatisha baada yake Mitume wengine. Na tukampa Isa, mwana wa Mariamu, hoja zilizo waziwazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Basi kila walipo kufikieni Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha, na wengine mkawauwa.”

Hii inarudiwa pia katika ayat za 253, 5:110 na sehemu nyingine nyingi. Katika sehemu zote hizo Allah ananukuliwa akisema alimtia nguvu Isa kwa Roho Mtakatifu. Lakini nini tafsiri ya wanazuoni wa kiislam juu ya Roho Mtakatifu? Sami Zaatari anaanza kwa kukubali kuwa
“Kama ilivyo katika Ukristo, sisi Waislam pia tunaamini katika Roho Mtakatifu, hata hivyo imani yetu katika Roho Mtakatifu ni tofauti kabisa na Ukristo katika jambo hili. Hata hivyo, ni nani huyu Roho Mtakatifu ambaye Koran inamsema?”[1] 
 Zaatari anaendelea na kutupa jibu ambalo wanazuoni wengine wa kiislam wanalitoa pale wanapofafanua juu ya “Ruh Al Quds”. Sami anahitimisha makala yake kwa kusema “Kwa hiyo kama unavyoona, Roho Mtakatifu hawezi kuwa mwingine ispokuwa malaika Jibril” [1]

Watakatifu wa Siku za Mwisho wanasema Ni Mungu Mwingine

Watakatifu wa siku za mwisho (LDS) nao wanaamini juu ya Roho Mtakatifu. Katika kitabu cha Momoni ambacho ni sehemu ya vitabu vyao kutoka kwa Mungu wao (mojawapo kikiwa ni Biblia), kitabu cha tatu cha Nephi sura ya 19 mstari wa 20 kinasema “ Baba, ninakushukuru wewe kwamba umewapa Roho Mtakatifu hawa niliowachagua...”. Lakini je, “watakatifu” hawa wanamtaja Roho huyu kama nani?

Tofauti na Baba na Mwana ambao wao wanaamini wana miili iliyotukuzwa, LDS wanaamini Roho Mtakatifu hana mwili [2]. Lakini pia wanaamini Roho Mtakatifu ni tofauti kabisa na Baba, na hivyo si Mungu mmoja nafsi tatu bali ni Mungu mwingine tofauti kabisa na Baba na Mwana [3]. McConkie na Joseph Fielding Smith, viongozi wakubwa wa “kanisa” hili wanasema “ Roho Mtakatifu ni mtu tofauti na aliyejitenga kabisa (distinct and separate) na Baba na Mwana”[4].

“Mashahidi wa Yehova” wanasema Roho ni Nguvu ya Mungu

Mashahidi wa Yehova hawaamini juu ya Utatu Mtakatifu na hivyo wanaamini Roho Mtakatifu ni nguvu tu ya Mungu Yehova. Wanaamini kuwa Mungu sio Utatu na kuwa hekaya na visasili vya Utatu viliundwa katika mji wa Nikea mwaka wa 325 B.K. [5] Wanaamini Mungu mmoja Yehova ambaye hajawahi kuonekana na kuwa Yesu Kristo ni Masihi, Mwana pekee wa Mungu aliyeumbwa mbinguni mabilioni ya miaka kabla ya Duni kuumbwa [6] ambaye pia ndiye malaika Mikael [7]

Hizi ni baadhi tu ya imani zingine nje ya Ukristo zinazojaribu kusema Roho Mtakatifu ni nani!

Kwanini ni nimeweka imani nyingine zinasemaje kuhusu Roho Mtakatifu? Kwa sababu baadhi ya Wakristo kwa kutojua maandiko wamejikuta wanaamini moja au mchanganyiko wa mafundisho haya. Na hii si kwa Bahati mbaya. Shetani anajua Roho Mtakatifu ndiye msaidizi wetu na ndiye anayetuwezesha kuishi maisha ya ushindi. Akituvuruga tukashindwa kumjua maana yake ni rahisi yeye kutushinda, na ndicho kinachotokea sasa. Kwa wanajeshi wanajua kuwa mawasiliano kati ya kamanda na kikosi chake yakiwa hayaeleweki ni vigumu sana kushinda vita hiyo.

Katika sehemu ya pili nitaangazia swali la Yesu kwa wanafunzi wake, Ninyi mnanisema mimi kuwa ni nani? Tutaangazia sisi kama watu wa Mungu, tunamsema Roho Mtakatifu kuwa ni nani?

Mpaka wakati mwingine, Mungu akubariki sana.
washirikishe wengine!
S.

Faharasa
[1] Sami Zaatari, Who is the Holy Spirit In Islam? - http://muslim-responses.com/The_Holy_Spirit_in_Islam/The_Holy_Spirit_in_Islam_
[2] Joseph Smith the Prophet, at Ramus, Illinois, April 2, 1843. https://www.lds.org/scriptures/dc-testament/dc/130.22?lang=eng
[3] What do Mormons believe about the Holy Ghost? Who is the Holy Ghost? http://www.mormon.org/faq/the-holy-ghost
[4] McConkie, Joseph Fielding, Holy Ghost http://eom.byu.edu/index.php/Holy_Ghost
[5] THE WATCHTOWER NOVEMBER 2009: Myth 4: God Is a Trinity, http://www.jw.org/en/publications/magazines/wp20091101/myth-god-is-a-trinity/