Wednesday, June 11, 2014

Mjue Roho Mtakatifu - 1 : Watu Husema Roho ni Nani?

Pengine umeshawahi kusikia maneno kama “Roho ameniambia” au “Sijisikii Roho akiniruhusu” na yanayofanana na hayo. Au hata umewahi kuona “mlokole” akifanya vituko kwa madai kuwa “Roho ameniambia”. Huyu Roho yukoje? Umewahi pia kujiuliza kwa nini pamoja na kwamba Roho ni mmoja lakini watu haohao wanaoongozwa na Roho wanapingana? Ukweli ni upi?

Katika makala hii nitakuletea mfululizo wa Neno la Mungu linasema nini juu ya Roho Mtakatifu. Kabla hatujaona Biblia inasema nini juu ya Mtu muhimu kabisa huyu, hebu tuangalie lile swali maarufu la Yesu “watu hunisema kuwa mimi ni nani?”. Je watu Husema Roho Mtakatifu ni nani?

Waislamu wanasema ni Malaika Jibril

Unaweza kuwa umeshtuka, lakini ukweli ni kuwa Koran inamtaja Roho Mtakatifu. Surat Al-Baqara ayat 87 (2:87) Koran inasema (msisitizo ni wangu)

“Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukafuatisha baada yake Mitume wengine. Na tukampa Isa, mwana wa Mariamu, hoja zilizo waziwazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Basi kila walipo kufikieni Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha, na wengine mkawauwa.”

Hii inarudiwa pia katika ayat za 253, 5:110 na sehemu nyingine nyingi. Katika sehemu zote hizo Allah ananukuliwa akisema alimtia nguvu Isa kwa Roho Mtakatifu. Lakini nini tafsiri ya wanazuoni wa kiislam juu ya Roho Mtakatifu? Sami Zaatari anaanza kwa kukubali kuwa
“Kama ilivyo katika Ukristo, sisi Waislam pia tunaamini katika Roho Mtakatifu, hata hivyo imani yetu katika Roho Mtakatifu ni tofauti kabisa na Ukristo katika jambo hili. Hata hivyo, ni nani huyu Roho Mtakatifu ambaye Koran inamsema?”[1] 
 Zaatari anaendelea na kutupa jibu ambalo wanazuoni wengine wa kiislam wanalitoa pale wanapofafanua juu ya “Ruh Al Quds”. Sami anahitimisha makala yake kwa kusema “Kwa hiyo kama unavyoona, Roho Mtakatifu hawezi kuwa mwingine ispokuwa malaika Jibril” [1]

Watakatifu wa Siku za Mwisho wanasema Ni Mungu Mwingine

Watakatifu wa siku za mwisho (LDS) nao wanaamini juu ya Roho Mtakatifu. Katika kitabu cha Momoni ambacho ni sehemu ya vitabu vyao kutoka kwa Mungu wao (mojawapo kikiwa ni Biblia), kitabu cha tatu cha Nephi sura ya 19 mstari wa 20 kinasema “ Baba, ninakushukuru wewe kwamba umewapa Roho Mtakatifu hawa niliowachagua...”. Lakini je, “watakatifu” hawa wanamtaja Roho huyu kama nani?

Tofauti na Baba na Mwana ambao wao wanaamini wana miili iliyotukuzwa, LDS wanaamini Roho Mtakatifu hana mwili [2]. Lakini pia wanaamini Roho Mtakatifu ni tofauti kabisa na Baba, na hivyo si Mungu mmoja nafsi tatu bali ni Mungu mwingine tofauti kabisa na Baba na Mwana [3]. McConkie na Joseph Fielding Smith, viongozi wakubwa wa “kanisa” hili wanasema “ Roho Mtakatifu ni mtu tofauti na aliyejitenga kabisa (distinct and separate) na Baba na Mwana”[4].

“Mashahidi wa Yehova” wanasema Roho ni Nguvu ya Mungu

Mashahidi wa Yehova hawaamini juu ya Utatu Mtakatifu na hivyo wanaamini Roho Mtakatifu ni nguvu tu ya Mungu Yehova. Wanaamini kuwa Mungu sio Utatu na kuwa hekaya na visasili vya Utatu viliundwa katika mji wa Nikea mwaka wa 325 B.K. [5] Wanaamini Mungu mmoja Yehova ambaye hajawahi kuonekana na kuwa Yesu Kristo ni Masihi, Mwana pekee wa Mungu aliyeumbwa mbinguni mabilioni ya miaka kabla ya Duni kuumbwa [6] ambaye pia ndiye malaika Mikael [7]

Hizi ni baadhi tu ya imani zingine nje ya Ukristo zinazojaribu kusema Roho Mtakatifu ni nani!

Kwanini ni nimeweka imani nyingine zinasemaje kuhusu Roho Mtakatifu? Kwa sababu baadhi ya Wakristo kwa kutojua maandiko wamejikuta wanaamini moja au mchanganyiko wa mafundisho haya. Na hii si kwa Bahati mbaya. Shetani anajua Roho Mtakatifu ndiye msaidizi wetu na ndiye anayetuwezesha kuishi maisha ya ushindi. Akituvuruga tukashindwa kumjua maana yake ni rahisi yeye kutushinda, na ndicho kinachotokea sasa. Kwa wanajeshi wanajua kuwa mawasiliano kati ya kamanda na kikosi chake yakiwa hayaeleweki ni vigumu sana kushinda vita hiyo.

Katika sehemu ya pili nitaangazia swali la Yesu kwa wanafunzi wake, Ninyi mnanisema mimi kuwa ni nani? Tutaangazia sisi kama watu wa Mungu, tunamsema Roho Mtakatifu kuwa ni nani?

Mpaka wakati mwingine, Mungu akubariki sana.
washirikishe wengine!
S.

Faharasa
[1] Sami Zaatari, Who is the Holy Spirit In Islam? - http://muslim-responses.com/The_Holy_Spirit_in_Islam/The_Holy_Spirit_in_Islam_
[2] Joseph Smith the Prophet, at Ramus, Illinois, April 2, 1843. https://www.lds.org/scriptures/dc-testament/dc/130.22?lang=eng
[3] What do Mormons believe about the Holy Ghost? Who is the Holy Ghost? http://www.mormon.org/faq/the-holy-ghost
[4] McConkie, Joseph Fielding, Holy Ghost http://eom.byu.edu/index.php/Holy_Ghost
[5] THE WATCHTOWER NOVEMBER 2009: Myth 4: God Is a Trinity, http://www.jw.org/en/publications/magazines/wp20091101/myth-god-is-a-trinity/








Tuesday, May 20, 2014

Siku Utakapovuta Pumzi yako ya Mwisho

Jabu alikuwa anatembea barabarani kwenda kumwona mkewe. Mkewe alikuwa na malaria na alikuwa amepumzishwa katika zahanati ya mtaa wao. Akiwa anavuka barabara ya mwisho kabla ya kuifikia zahanati, ghafla anasikia watu wakipiga kelele za uoga. Alipogeuka akaona lori la mizigo limeacha barabara likimfuata. “mamaaa!” akapiga kelele ukijaribu kulikwepa. Kitu cha mwisho anachokumbuka ni kishindo kikubwa na maumivu makali.

Baada ya hapo alijihisi kama anajivua toka katika mwili, mithili ya nyoka anayejivua gamba. Ghafla akawa kama anazama katika giza kubwa na macho yake yakififia mithili ya taa hafifu katika ukungumzito. Sambamba na hilo alianza kuhisi joto likiongezeka na kuwa kali na harufu mbaya ya moshi wa yai lililooza ukiibuka. Kwa sabau alikuwa mtaalam wa kemia, Jabu alijua ni salfa inayoungua. Hakuweza kupumua vizuri kabisa kwa moshi mzito na harufu kali. Hofu kuu ilimshika, na hakuelewa ch kufanya. Kufumba na kufumbua, Jabu alikuwa katika eneo kubwa ambalo hakuweza kujua limeanzia wapi wala kuishia wapi. Alichoona ni moshi mzito na giza nene. Alichosikia ni sauti nyingi sana zikilia kwa maumivu makali. Hakujua kama alikuwa analia au anagugumia, lakini alijua kwa hakika alikuwa akisaga meno kwa maumivu makali aliyoyasikia.

Jabu alikumbuka siku moja kanisani ambapo mchungaji wake elielezea sehemu inayoitwa kuzimu, ambayo inafanana na hapa alipo. “hapana, sio kwamba panafanana, ndio penyewe!” alijisemea moyoni. Jabu alianza kujilaumu kwa nafasi zote alizozipoteza. Akakumbuka watu waliomsihi kwa machozi na kumwonyesha njia impasayo, lakini aliwadharau na kuwapuuza. Sasa alikuwa katika mahali alipodhani hapakuwahi kuwepo, na alijua hakuna jinsi ya yeye kutoka. Alitamani iwe ndoto, lakini haikuwa hivyo.

Aliwashukuru wale watu walioonekana vichaa njiani wakidharauliwa,kwa upendo wao. Moyo wake ulimuuma sana. Akamkumbua rafiki yae Mwema, aliyekuwa akienda kanisani kila siku na hakuchukua muda kumuonya. “Pengine angesema kwa kuwa ni rafiki yangu ningemsikia”. Namchukia kwa alilolifanya. Alitamani arudi akawonye rafiki zake kuwa kuzimu ipo, na sio mahali pa kwenda, lakini hakuwa na namna. Kifo kilikuwa kimemtenga na mahali pa walio hai, tumaini na wema vimemwacha. Aliungana na aliowakuta huko kulia kilio cha kukata tamaa......!

Kuzimu na Jehanamu Ipo
Watu wengi wanadhani hii ni hadithi ya kufurahisha kama ilivyo hekaya za abunuwasi au alfu lela-ulela. Shetani, adui wa roho yako anajua pia kama ataifanya Jehanamu na Ziwa la mot vionekane ni visasili, atakufanya uvipuuze. Lakini hebu jiulize: unawekeza nguvu na raslimali zako kiasi gani kuhakikisha unaishi maisha mazuri hapa duniani? Umesoma vitabu vingapi vya “jinsi ya kufanikiwa” au vifananvyo na hivyo? Mara ngapi umefanya hili na lile kuhakikisha unafanikiwa? Au ni miaka mingapi umekuwa shuleni lengo likiwa ni ufanikiwe? Halafu jiulize umetumia raslimali kiasi gani kujua utakakokwenda baada ya miaka michache sana uliyo nayo? Utagundua unatania!

Neno la Mungu lipo wazi kuwa baada ya kifo ni hukumu (Waeb 9:27). Ukifa faili la maisha yako linakuwa limefungwa na mahali pa kwenda pameamuliwa. Mungu aliyeumba mbingu na nchi, aliweka utaratibu wa sisi kuishi katika dunia yake (Kutoka 20:3-17). Alikataza watu kusema uongo, kuiba, kuwa na miungu, katika dunia yake. Na aliweka adhabu kwa wavunjaji wote, nayo ni Ziwa la moto (Ufun 21:8, 1 Kor 6:9). Baada ya kufa nafsi yako itakwenda “selo” kusubiri siku ya kusomewa hukumu yako. Huko ndiko kuzimu ambako hakuna raha bali ni maumivu (Luke 16:22-24). Utakuwa ukijielewa na maumivu utayasikia. Hili ni tone tu ukilinganisha na hukumu yenyewe.

Neno liko wazi kabisa kuwa iko siku Mungu ameiandaa kwa ushahidi kabisa (tazama somo hili kwa makala inayohusiha hilo). Wengi wanadhani Mungu ni kama mjomba Santa, akileta zawadi za Krismasi. Lakini kwa kweli wengi watapigwa namshangao watakapokutana uso kwa uso na Muumba wao. Mungu anatisha kwa kuwa ni mkuu mno. Yeye Mungu “ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. ” (1Tim 6:16). Mpendwa wangu, Mungu sio yule uliyedanganywa. Na kwa hasira yake aliiandaa Jehanamu ya moto kwa shetani na wote watakaomfuata katika uasi wa sheria ya Mungu.

Baada ya Mungu wa haki kukuonyesha yote uliyofanya na jinsi bila soni ulivyovunja amri zake atakuhukumu kwenda katika ziwa la moto. Wewe na selo mtatupwa katika gereza la mwisho, yaani Ziwa la moto (Ufun 20:14-15). Hapo ni kilio na kusaga meno milele maana huko “funza wao hafi, wala moto hauzimiki” (Mark 9:46, Luk 13:28).

Jehanamu siyo sehemu ya kwenda mpendwa, na Mungu siyo wa kukutana naye kama jaji, maana anatisha. Yesu mwenyewe alionya kuwa kama “mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum” (Mark 9:45). Jehanamu ni mahali pabaya kiasi kwamba nakushauri kama gari lako, mke, mume au chochote kitakuwa sababu ya wewe kwenda huko kitupe.

Yawezekana umeashaanza “kutenda mema” ili upate sababu ya Mungu kukuruhusu uende mbinguni. Nikuhakikishie hata utende mema kiasi gani hayafuti makosa uliyofanya, na kujaribu kumhonga Mungu matendo yako ili “asahau” makosa yako ni kosa kubwa zaidi. Mungu anayaita matendo yako hayo kuwa ni kama “nguo iliyotiwa unajisi” (Isay 64:6). Usijaribu kumpa Mungu rushwa ya matendo mema, hataipokea! Na usijidanganye kwamba Mungu atakusamehe”ukitubu”. Jaribu kumwambia hakimu nimeiba ila ninatubu, nisamehe uone. Kama mwanadamu anasimamia sheria za wanadamu vema, unadhani Mungu si zaidi kusimamia sheria zake mwenyewe?

Waweza kuwa unajiuliza kuwa “kama ni hivyo nifanye nini sasa ili nami niiepuke Jehanamu?” Jibu ni kuwa huna cha kufanya. Mungu alifanya mwenyewe. Mungu alitwaa mwili akakaa kwetu (Yoh 1:14) akaishi maisha matakatifu na kufa kwa ajili yetu, akilipa deni la hatia yetu: ili sisi tulio wa dhambi na tuliohukumiwa Jehanamu tupate kwenda Mbinguni. Yesu alilipa deni la dhambi zote hivyo hakuna sababu ya wewe kwenda Jehanamu. Unachopaswa kufanya ili deni la uasi wako lifutwe ni kumkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa alikufa kwa makosa yako na kuomba akusamehe na kukuosha dhambi zako, utaokoka!

Pamoja na kuwa Mungu amelipa, kuna watu watakwenda huko kwa sababu ya kiburi. Ukikataa neema ya Mungu leo utajutia siku moja. Na siku hiyo yaweza kuwa hata leo. Je wajua kitakachofuata dakika tatu zijazo? Usiwe mpumbavu kama Jabu, kupoteza nafasi hii adimu.mkiri Yesu leo akuokoe na adhabu kali ya Mungu wa Mbinguni.

Bwana Yesu na akubariki,
Maranatha!

Saturday, May 3, 2014

Swali #1 – Je Daniel Alikosea Jina la mfalme wa Mwisho wa Babeli?


Swali
Danieli Sura ya Tano inasema Belshaza ndiye alikuwa mfalme wa mwisho wa Wakaldayo. “Usiku huo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa. Na Dario, Mmedi, akaupokea ufalme, naye umri wake alikuwa na miaka sitini na miwili.” (Dan 5:30-31). Katika maandishi ya wanahistoria wengine haiko hivyo na kutoka katika maandiko ya kale tunajua kuwa Nabonidus ndiye alikuwa mfalme wa mwisho wa Babeli kabla ya uvamizi wa Wamedi na Waajemi uliopelekea mwisho wa dola ya Wakaldayo. Kama Daniel alikuwepo enzi hizo aliwezaje kukosea kitu kilicho wazi hivi? Na kama alikosea jambo rahisi kama hili tutaaminije kama kitabu hiki sio utunzi wa Mtu fulani baada ya matukio (ambapo ni rahisi kukosea kwa kuwa hakuwepo)?

Jibu
Danieli ni moja ya vitabu vya Biblia ambavyo vimeshambuliwa sana, na kwa sababu ambayo mtu yeyote aliyeyasoma haya au kuyatafiti atayaelewa. Wenye kushuku na wasioamini Biblia hawana jinsi ya kutimiza malengo yao bila kushambulia vitabu hivi kwa kuwa vimejaa uthibitisho kuwa Biblia haiwezi kuwa Neno la mwanadamu kwa kuwa imetabiri kwa kina matukio, na mambo na falme kwa usahihi kiasi kwamba hakuna namna mwanadamu angeweza kuandika. Moja ya vitabu vya Biblia vyenye unabii huu wa kutisha ni kitabu cha Daniel.

Mashambulizi hayakuanza jana wala juzi. Polfili, mwanafalsafa wa kipagani ni moja kati ya watu wa mwanzo kabisa kukishambulia kitabu hiki. Hatujabakiwa na kazi zake ila tunaweza kujua kupitia wanatheolojia waliokuwa wakijibu mashambulizi haya. Mathalani, Jerome katika maoni yake juu ya kitabu cha Danieli anasema

Polfili aliandika katika kitabu chake cha kumi na mbili dhidi ya unabii wa Danieli, akikana kwamba kiliandikwa na mtu ambaye kitabu hiki kimepewa jina lake, ila mtu mwingine aliyeishi Yudea wakati wa Antiokasi aliyeitwa Epifania. Na zaidi ya hayo anadai kuwa “Danieli” hakutoa unabii juu ya wakati ujao kama ambavyo alisema juu ya wakati uliopita, na mwisho kuwa chochote alichosema mpaka wakati wa Antiokasi kilikuwa ni historia thabiti, wakati chochote alichojaribu kubahatisha zaidi ya wakati ule kilikuwa si kweli, kama ambavyo asingeweza kujua wakati ujao

Mashambulizi ya leo juu ya kitabu hiki aidha ni marudio ya mwanafalsafa huyu, yakiwa yamepakwa rangi ya ukisasa au ni mapya yakifuata msingi wa Polfili. Kitu kimoja ambacho kilimfanya huyu mwanafalsafa afikie hitimisho lake hili ni kuwa maandiko katika Danieli yalitimia hata nukta. Kwa akili timamu ya kawaida kabisa, hakuna namna Danieli angeweza kujua mambo yajayo kwa usahihi hivyo: alijua haukuwa ubahatishaji. Kwa hiyo alibakiwa na njia mbili za kufuata. Aidha Daniel aliandika karne ya 6 K.K au atengeneze namna ya maelezo kuwa ni uhuni uliofanywa baada ya matukio. Bahati mbaya alichagua njia ya pili ambayo siyo ya kweli.

Nikirudi kwenye swali la leo ambalo wengi wa wanaolitumia kama ngao ya kukwepa kuiamini Biblia hufuata nyayo za Polfili, limetokana na kutokuelewa historia na kutojishughulisha. Japo wengi wamelikimbia swali hili na hawalitumii tena, bado wapo wenye kushuku wanaolitumia ili pengine kuwapotosha Wakristo wachanga na wengine wasiojua. Mfano katika maandiko yao, “Skeptic Annotated Bible” wameandika “mfalme wa mwisho wa Babeli alikuwa Nabonidasi aliyetawala toka 556 mpaka 539 and aliyeshindwa na Koreshi. Alikuwa Nabonidasi na si Belshaza aliyekuwa wa mwisho katika wafalme wa Babeli.”

Kwanza hatutumii historia kujaribu kuhukumu Neno la Mungu. Wanahistoria nje ya Biblia wamekuwa wakikosea mambo mengi na hata majina mbalimbali, na unapofanyika ugunduzi wa mambo ya kale, Biblia imekuwa ikithibitishwa kuwa sahihi. Hata hivyo, kwa hili historia ya nje ya Biblia iko sahihi, na Biblia haijakosea. Mfalme wa mwisho wa Babeli hakuwa Belshaza bali Nabodinasi. Na ndio maana Biblia inasema yafuatayo baada ya Danieli kutafsiri maneno yaliyoandikwa na kiganja mbele ya Belshaza:

Ndipo Belshaza akatoa amri, nao wakamvika Danieli mavazi ya rangi ya zambarau, wakatia mkufu wa dhahabu shingoni mwake, wakapiga mbiu kutangaza habari zake, ya kwamba yeye ni mtu wa tatu katika ufalme. (Danieli 5:29)

Hapa Daniel anapaswa kuwa mtu wa tatu kwa kuwa tayari Belshaza alikuwa ni mtu wa pili na kwa hiyo alikuwepo mtu wa kwanza, naam, naye ni mfalme Nabodinasi. Katika andiko la Nabonidus mwenyewe linalofahamika kama "Nyakati za Nabodinasi"[1] tunajua kuwa "Mfalme alitumia miaka kumi huko Araba na akaacha Babeli ikisimamiwa na mwana wake Bel-Shar-Usur [Belshaza]". Kwa hiyo wakati nabonidasi hakuwepo Mfalme wa Babeli alikuwa Belshaza lakini akiwa mtu wa pili na si wa kwanza. Kwa hiyo Biblia hapa ipo sahihi kwa kuwa Danieli, aliyeandika kitabu hiki alishuhudia aliyoyaona.

Kuna Jambo kubwa zaidi ya hili la Danieli kuwa sahihi. Nalo ni kuwa Mungu aliyesema na Danieli, Yeye aliyeumba mbingu na nchi, ametenga siku awahukumu wanadamu wote sawasawa na matendo yao. Mungu atatuhukumu si kwa matendo tu yaliyo maovu bali hata mawazo na nia ovu zote. Siku hii ya kutisha inakuja na njia pekee ya kuepuka hukumu hii ni kujisalimisha kwa Yesu Kristo, yeye aliye mwokozi wa wanadamu wote. Leo hii umlilie yeye, utubu na kugeuka toka njia zako mbaya. Naye atakusamehe makosa yako na kukupa uzima wa milele. Kumbuka Yesu anakuja, furaha kwa watu wake na huzuni, kilio na kusaga meno kwa waliomkataa.

Maranatha!

[1] http://www.britishmuseum.org/explore/highlights/highlight_objects/me/c/cuneiform_fall_of_a_dynasty.aspx

Friday, April 18, 2014

Moyo wa Pasaka - Sehemu ya Mwisho

Katika sehemu ya kwanza tuliona kifupi ni nini moyo wa Pasaka kibiblia. Sehemu hii ya mwisho tutamalizia kuona kwa ndani zaidi maana ya pasaka kwako wewe binafsi. Karibu tuendelee...

Pasaka Ina Maana Gani Kwako?
Moyo huu wa pasaka una sura mbili. Sura ya kwanza ni ya tabasamu la bibi harusi akimsubiri Bwana harusi arudi mara amalizapo kujenga nyumba watakayokaa huko kwa Baba wa Bwana harusi. Bibi harusi anasubiri kwa hamu akichungulia chungulia aone kama Bwana wake yuaja. Akijiandaa na kuhakikisha yu msafi ili sekunde ile Bwana harusi atakayokuja amkute tayari. Sisi kama kanisa la Kristo, ambao tumemkiri na kumwamini Yesu awe si tu Mwokozi kwetu bali mtawala wa maisha yetu na bosi mkuu, tunaitwa ni bibi harusi, ambapo tunapaswa kuishi kwa utakatifu kama "bikira safi" (II Kor 11:2). Na ndipo tunasubiri siku ile ambapo tutasahau taabu na maumivu, na magonjwa na yote ya dunia hii, siku ile kuu ya kukutana na Bwana harusi, maana:

"Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele" (1Th 4:16 - 17)
 
Picha ya pili ni ya huzuni, mashaka na kukosa amani. Amini usiamini, pamoja na Mungu kuingia gharama ya kulipa deni la dhambi kuna watu wako wanaugulia maumivu Kuzimu, na wapo kati yetu, pengine hata ikawa ni wewe unayesoma, ambao wataingia Jehanamu ya moto. Kiburi cha kutotaka kushuka mbele za Muumba wako na kupenda kwako dhambi vitakuangamiza. Kwako mtu wa namna hii pasaka ni ujumbe wa machozi na majonzi.

Ina maana kuwa Yesu atakapokuja kuchukua bibi arusi wake, hautakuwa mmojawapo. Ni kweli unajidanganya kuwa wewe ni Mkristo huku ukijua toka katika moyo wako kuwa Yesu hakujui. Ndio, endelea kujifariji ila siku yaja ambapo Yesu anasema "Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu" (Matt 7:23). Usisherekee Pasaka maana moyo wa pasaka kwa watu wa aina yako ni tangazo la ole!

Si kwamba tu utakosa nafasi ya bibi arusi, lakini pia utapitia wakati mgumu sana duniani ikitokea ukawa hai. Mungu atauhukumu ulimwengu kwa dhiki kubwa sana ambayo haijawahi kuwepo wala baada ya hapo haitakuwapo. Itakuwa ni zaidi ya vita zote mbili za dunia. Na mwisho Yesu huyu ambaye tunasherekea pasaka leo ataweka kiti cha Enzi cha hukumu ili akuhukumu kwenda ziwa la moto, naam "Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto" (Ufu 20:15). Mpaka sasa sijaelewa unasherekea nini katika hali kama hii!

Ndio, sitaki nikufariji kwa maneno mfu maana Biblia iko wazi kuwa "Kwa maana [Mungu] ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu" (Mdo 17:31), ufufuo wa Yesu ambao unapanga kuusherekea ni uthibitisho kuwa utahukumiwa na Mungu kwenda ziwa la moto hakika, ni kipi cha kusherekea kwako?

Ushauri Mwema
Kwako wewe uliye kati ya bibi arusi, jiweke safi. Tengeneza mavazi yako ili akija sasa, uwe tayari kwenda nae kwa Baba yake. Kumbuka atakuja kuchukua kanisa safi, lisilo na makunyazi wala mawaa. Yesu Kristo anakuja!

Kwako wewe usiyeokoka, fanya hima ufanye amani na Muumba wako. Maana "ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka" (Rum 10:9). Unasema utafikiria? Hujui kama muda huu unaposoma hapa unaweza kuwa umebakiza dakika au hata sekunde chache kumaliza maisha yako? kumbuka baada ya kifo ni hukumu (Ebr 9:27). Fanya Uamuzi wa busara sasa. Chagua kuokoka na hasira ya Mungu ili pasaka iwe ni tabasamu kwako. Kwamba tutakaa na Mungu milele, ndio kusudi la Mungu na moyo wa pasaka!

Mungu akutunze na kukubariki!
Stefano


MOYO WA PASAKA - Sehemu ya I

Kwa wengine pasaka ni wakati wa mapumziko ya kifamilia na kutafakari maendeleo yao, walipojikwaa na wanapoelekea. Kwa wengine ni Wakati wa "kuponda mali, kufa kwaja" na wapo ambao pasaka ni wakati wa kufikiria kuhusu dini zao na kuangalia namna wanayoweza kujitengenezea mazingira ya kuzikwa na dini zao wakifa. Lakini kwa wengine pia ni wakati wa kusherekea ushindi wa Bwana na Mwokozi wao, Yesu Kristo.

Makundi yote haya, isipokuwa la mwisho, hawako sahihi. Pasaka ni wakati mzuri wa kusherekea ushindi wa Mwokozi wetu Yesu Kristo. Hili ni jambo la muhimu sana ambalo bila hilo hakuna Pasaka. Swali la msingi ambalo nilikuwa nalitafakari hata kunisukuma kuandika makala hii fupi sana ni hili "nini hasa moyo wa Pasaka"? Ni kweli ni siku ya kufurahia ushindi, na ni kweli kuwa Ukombozi wa Mwanadamu hautenganishwi na tukio hili. Lakini ni nini moyo wa Pasaka hasa? Majibu ya tafakari hii ndiyo ninataka nikushirikishe.

Mfululizo wa Matukio
Kabla sijaweka kile nimejifunza leo hebu tuangalie kifupi matukio kuelekea pasaka. Yesu na wanafunzi wake wako katika chakula cha jioni, huku shetani akiwa amekwisha uteka moyo wa Yuda. Yesu hali akijua anahesabu masaa kabla ya kipigo, maumivu na mateso, anawafundisha wanafunzi wake kutumikiana, akifanya kazi iliyofanywa na watumwa, kuosha miguu ya wanafunzi wake. Petro anajaribu kuzuia hili (Yoh 13:6-9) Bwana anamkemea na kuendelea na kazi yake hiyo. Mwisho Yesu anawaambia wanafunzi kuwa Yuda Iskariote atamsaliti na Yuda, kwa kuingiwa na shetani, anakwenda zake kulifanya alilo kusudia moyoni mwake. Haya yote ni mfululizo wa matukio kuelekea Pasaka, sura ya 13. Baada ya haya yote, inafuata sura ambayo ina moyo hasa wa Pasaka!

Moyo wa Pasaka na kusudi la Mungu
Moyo wa pasaka umeambatana na kusudi la Mungu la milele. Kabla hajaumba chochote, Mungu alijua mambo yote ambayo yatatokea katika historia ya mwanadamu. Kwa sababu ya ufahamu wake wa milele, usio na mwisho, Mungu aliumba akiwa na kusudi. Kusudi hili ndio moyo wa Pasaka. Kifo cha Yesu Kristo, na kufufuka kwake, vyote hivi ni njia za kufikia kusudi hili: Mahusiano ya Mungu na mwanadamu. Hebu tusome maneno ya Yesu mwenyewe katika sura hii ya 14 ya Yohana:
"Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo" (Yoh 14:1 - 3)
 
Yesu anawaambia wanafunzi wake kuwa wasifadhaike, na sababu ni kuwa anakwenda kuwaandalia mahali katika makao ya mbinguni. Mstari huu unatupa moyo wa pasaka ni Mungu akae na wanadamu. "Maana naenda kuwaandalia mahali", ni ahadi nzito kabisa kuwa ipo siku inakuja ambapo wote tulio wanafunzi wa Yesu Kristo tutakaribishwa naye kwa Baba yake. Ndiyo, Yesu Mwenyewe anasema "nitakuja tena niwakaribishe kwangu". Huu ndiyo moyo wa Pasaka.

Mungu alipomuumba mwanadamu, alikuwa na ushirika naye wa namna ya ajabu kabisa. Hata pale Adamu na mkewe walipoasi sheria ya Mungu bado Mungu aliwatembelea. "Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga" (Mwa 3:8). Mungu alimuumba Mwanadamu ili awe na ushirika nae, na ndio maana akamuumba kwa mfano Wake na sura Yake (Mwa 1:26-27). Kwa sababu ya kusudi hili Mungu alitembea na Henoko miaka 300 (Mwa 5:22), Nuhu, Ibrahimu, Daudi na wengine wengi. Ibrahimu, Biblia inatuambia, " alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu" (Ebr 11:10). Ni Mji huu ambapo Mungu atakamilisha kusudi lake la milele, ambapo "maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu" (ufu 21:3).

Yesu anaongelea makazi haya ambayo kwa milenia mbili amekuwa akituandalia, ili alipo nasi tuwepo. Huu ndio moyo wa Pasaka. Mungu aliamua kumtoa mwanawe wa pekee ili afe, ili kwa kifo chake Yeye asiye na hatia, abebe hatia zetu zote na tuweze kuwa na uhalali kwa kifo na damu yake, kuingia katika mji huu. Mauti ya msalaba na ufufuko wa Yesu ulikuwa ni kutimiza kusudi hili na ndio moyo halisi wa pasaka!

Katika sehemu ya pili tutamlizia kuona kwa nini na jambo hili lina maana gani kwako.
Amani ya Kristo, na Neema yake kuu iwe nawe, amen!
Stefano

Soma Sehemu ya Pili hapa


Wednesday, April 16, 2014

Historia Nyuma ya Utenzi wa Kaa Nami

“Kaa nami ni usiku sana, Usiniache gizani Bwana, Msaada wako Kwangu haukomi, Nili peke yangu Bwana Kaa nami” ni sehemu ya maneno ya wimbo huu unofikirisha na kutukumbusha kuwa tunapita tu hapa duniani na kuwa bila msaada wa Bwana Wetu, hatutashinda wala kufika mwisho kwa salama. Lakini ni nani aliuandika wimbo huu, na ni nini kilimsukuma kuandika maneno hayo?

 Sehemu ya Wimbo wa Kaa nami (Abide with me) ulivyoandikwa na mkono wa H.F. Lyte. Ukitaka nakala ya wimbo wote wasiliana nami!










Henry Francis Lyte alizaliwa mnamo tarehe 1 Juni mwaka 1793 akiwa sehemu ya familia ya Bwana Tomaso na Anna Maria Lyte huko Ednam, Uskochi. Tomaso baadaye aliamua kuitelekezafamilia na Anna akahamia mjini London, Uingereza na alifia huko, yeye na mwanawe mdogo. Akiviona vipawa vya Henry, Dkt. Robert Burrowes aliamua kumuasili na kumlipia ada na Henry akasoma Trinity College mjini Dublin huko Ireland akizama katika Ushairi.

Mwaka 1815 akaingizwa katika huduma ya kanisa La Uingereza (Anglican Church) na akatumikia parishi kadhaa huko Ireland na magharibi ya Uingereza. Miaka miwili baadae alikuwa ni kasisi wa Marazion, Cornwall, alipomwona na kumwoa Anne Maxwell, aliyekuwa na miaka 31 huku Henry akiwa na miaka 24 tu. Hata hivyo ndoa yao ilikuwa ya furaha na ulikuwa wakati mzuri wa Henry kusahau maumivu ya maisha yake.

Akiongea Kilatini, Kiyunani na Kifaransa, Henry alihamia mji wa wavuvi ulioitwa Brixham, mwaka 1824, na kanisa la Brixham lilikua kwa kasi baada ya kufika kwa Henry, kijana mtanashati, mshairi mzuri na mtu mwelewa wa mambo, mwanazuoni. Henry alihudumu kanisa hilo kwa miaka 23.

Imani ya Henry kwa kiasi kikubwa iliathiriwa na Abraham Swanne. Henry alikuwa akimhudumia Mchungaji Abraham, Jasiri mtu wa imani na asiyeogopa kifo. Mchungaji Abrahamu alikuwa akiuguzwa na Henry, akiwa katika hali ya kufa.

Akisumbuliwa na Mkamba na Pumu, na baadae Kifua kikuu, Henry alidhoofu sana. Hata hivyo alibaki kuwa mwenye furaha katikati ya dhiki hii.Mke wake Anna alijitahidi kutunza fedha na kuweza kumpeleka nchi za joto, Ufaransa na Italia wakati wa baridi.

Akiwa na miaka 54, akiwa amedhoofu, Henry alihubiri mahubiri yake ya mwisho. Katika mahubiri hayo ambapo aliwaaga watu wake na kuwakumbusha kuwa sote tutakufa na kuwa wale wote walioishika imani katika Kristo Yesu wamejiandaa vyema kabisa kukutana na kifo.

“Nasimama haba kati yenu leo, kama aliye hai toka kwa wafu, kama nitaweza kuliweka hili katika fikra zenu, na kuwafanya muwe tayari kwa saa ile kuu ambayo itawajia wote, kujitambulisha na kifo cha Kristo” . Baada ya ibada yake ya mwisho, Henry alikaa na kuandika mashairi ambayo leo tunayafahamu kama Utenzi uitwao “kaa nami”!

Wiki kumi baadae, Novemba 20, 1847, Franscis Henry Lyte alikwenda kupumzika kwa Baba Mbinguni. Utenzi wa kaa nami umekuwa ukiimbwa katika mashindano mbalimbali, ikiwamo kombe la Dunia kabla hawajauweka kando.

Bwana anatumia hata wadhaifu wa afya, kufanya mambo makubwa. Maisha ya Lyte yakutie moyo ufanye kazi ya Bwana bila visingizio



-Maranatha!

Vyanzo:
  1. http://www.poemhunter.com/henry-francis-lyte/
  2. Biography and hymns of Henry Francis Lyte (1793-1847), http://www.cyberhymnal.org/
  3. Dying Henry Lyte Asked God to Stay Near, http://www.christianity.com/church/church-history/timeline/1801-1900/dying-henry-lyte-asked-god-to-stay-near-11630479.html


Friday, April 11, 2014

Kufufuka Kwa Yesu Kristo

Haya ni maadiko niliandika Aprili 11, 2009. Nimeona nishirikiane nanyi hapa tubarikiwe sote. Kama yakikufaa, washirikishe wengine. Huu ni ufupisho wa makala ndefu niliyoandika mwaka huohuo. Kama utaihitaji naweza kukutumia

Kufufuka kwa Yesu Kristo ni moja ya mambo ambayo yamekuwa ni chanzo cha mjadala dunia nzima. Dini nyingine zimedai kuwa Yesu hakufa na hivyo kumaanisha hakufufka. Wanazuoni wengine wamejaribu kuhusianisha kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo kama mwendelezo wa imani za kipagani zilizokuwapo kabla ya ukristo, na mengine mengi, kadha wa kadha.

Kwetu sisi wakristo, imani Yetu inasimama au kuanguka katika kufufuka kwa Yesu Kristo. Kwa kufufuka kwake, aliushuhudia ulimwengu kuwa Yeye ndiye Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele na mfalme wa amani kama Ilivyotabiriwa na manabii (Isaya 9:6). Kushambulia kufufuka kwa Kristo Yesu, ni kushambulia kiini cha ukristo kama mtume Paulo alivyoandika

“Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tumemtumainia Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote” (1Wakorintho 15:17-19)

Maneno ya Paulo yana maana kubwa wapendwa. Kama Kristo hakufufuka, tumepoteza muda bure, kuomba kwa Mungu mfu, tumejinyima bure kwa ajili ya mtu aliyekufa miaka 2000 na zaidi iliyopita, na tumaini letu kuwa Yesu anatuandalia makao nayakuwa atakuja kutuchukua tena ni bure! Je waona sasa ni jinsi gani imani yetu inasimama au kuanguka katika kufufuka kwa Kristo? Naam, kama Kristo hakufufuka, ni heri tuishi na kuponda mali maana kufa kwaja!

Habari njema ni kuwa Kristo Yesu alifufuka katika wafu! Historia inashuhudia hivyo, na neno la Mungu linashuhudia hivyo. Wanahistoria kama Luka, Mathayo, Yohana, Josephus, Tacitus na wengine wengi wameandika mambo mbalimbali kuhusu kifo na kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo. Lakini hi ina maana gani kwetu? Kwa nini Yesu alikufa? Ni kwa ajili ya dhambi zetu! Unaweza sema utakwenda mbinguni kwa kuwa u mwema. Ndio, inawezekana u mwema ukilinganisha na Adolf Hitler. Lakini je Mungu anakuonaje? Mwema? Kama jibu ni ndio, hili ni jaribio waweza kufanya ili kujiona u mwema kiasi gani!

Hebu jiulize na iache dhamiri yako itoe jibu. Ulishawahi kusema uongo, hata mara moja katika maisha yako yote? Kama jibu ni ndiyo, wewe ni mwongo. Ulishawahi kuiba mali yoyote bila kujali thamani yake? Kama ndiyo, wewe ni mwizi. Ulishawahi kuzini? Hii ina maana hata kama ulimwangalia mtu ukamtamani, umezini naye moyoni mwako (Mathayo 5:27-28)? Kama ndio, wewe ni mzinzi. Umewahi kuua? Yesu alisema kumchukia nduguyo bila sababu ni kuua (Mathayo 5:21-22). Kama ndiyo wewe ni muuaji. Hivi ni vigezo vine kati ya kumi ambavyo Mungu atakuhukumu siku ya mwisho. Sikia Neno la Mungu linachosema:

“Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawaaturithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi , wala, wala watukanaji ”(1 Wakorintho 6:9-10)”.
Kwa kifupi, viwango vya Mungu viko juu sana, na wote tumetenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu (Warumi 3:23). Sote tumehukumiwa kwenda katika ziwa la moto, maana baada ya kifo hukumu (Waebrania 9:27). Mbele za Mungu Baba, aliye mtakatifu sana, hatufai na haki yetu itokanayo na matendo yetu ni kama takataka mbele za Mungu (Isaya 64:6). Mbele ya hakimu wa haki, hatuna la kujitetea. Tumetenda dhambi hali tukijua maana Mungu ameandika sheria yake katika mioyo yetu (Warumi 2:14-16). Kwa hiyo, kwa binadamu wote, ziwa la moto haliepukiki!

Habari njema ni kuwa, Yesu Kristo alikuja kulipa deni hili. Aliishi maisha Makamilifu ambayo mimi na wewe hatuwezi kuishi. Lakini pia alikufa, katika sehemu yetu, ili sisi tuishi. Kwa hiyo wote wanaokubali kazi yake msalabani na kufufuka kwake, wanahesabiwa haki, si kwa wema wao, bali kwa haki iliyo ndani ya Kristo Yesu (1Petro 3:18).

Mfano unaofanana kidogo ni huu, mko mbele ya mahakama, mnadaiwa deni kubwa sana ambalo hamwezi kulilipa. Hukumu imetolewa, mlipe deni au mwende kifungo cha maisha na viboko kila siku. Hamna uwezo wa kulipa na mnasubiri mpelekwe kifungoni. Ghafula hakimu anasimama na kusema, hizi hapa ni pesa toka mfukoni kwangu, nimelipa deni lote. Ila ili uhesabiwe umelipiwa sharti ukiri kwa kinywa na kuamini kwa moyo kuwa mimi hakimu nimekulipia deni lote. Hicho ndicho Yesu Kristo alifanya!

Bila ya Kristo, tunadaiwa, na mbele ya Mungu. Waanzilishi wa imani/dini nyingine zote hawakulipa deni la dhambi. Ni Yesu pekee alilipa. Mwamini Yesu Kristo leo upate kulipiwa deni lako na kuhesabiwa haki wewe ambaye bado hujampokea Yesu. Ni rahisi na haihitaji gharama. Ni lazima udhamilie moyoni kuacha dhambi na kuishi kwa ajili ya Kristo (Utubu). Biblia inasema ukimkiri Yesu kwa kinywa chako NA kuamini katika moyo wako kuwa Mungu alimfufua toka wafu UTAOKOKA. Chaguo ni lako!

Na wewe mpendwa ambaye umempokea Yesu Kristo, hili ndilo tumaini pekee ulilo nalo, ya kwamba Yesu alifufuka na anaandaa makao na atakuja kutuchukua muda wowote. Uwe tayari kwa siku hiyo(Yohana 14:2)

Neema ya Kristo na amani kutoka kwa NIKO iwe nanyi, Amina!