Friday, April 11, 2014

Kufufuka Kwa Yesu Kristo

Haya ni maadiko niliandika Aprili 11, 2009. Nimeona nishirikiane nanyi hapa tubarikiwe sote. Kama yakikufaa, washirikishe wengine. Huu ni ufupisho wa makala ndefu niliyoandika mwaka huohuo. Kama utaihitaji naweza kukutumia

Kufufuka kwa Yesu Kristo ni moja ya mambo ambayo yamekuwa ni chanzo cha mjadala dunia nzima. Dini nyingine zimedai kuwa Yesu hakufa na hivyo kumaanisha hakufufka. Wanazuoni wengine wamejaribu kuhusianisha kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo kama mwendelezo wa imani za kipagani zilizokuwapo kabla ya ukristo, na mengine mengi, kadha wa kadha.

Kwetu sisi wakristo, imani Yetu inasimama au kuanguka katika kufufuka kwa Yesu Kristo. Kwa kufufuka kwake, aliushuhudia ulimwengu kuwa Yeye ndiye Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele na mfalme wa amani kama Ilivyotabiriwa na manabii (Isaya 9:6). Kushambulia kufufuka kwa Kristo Yesu, ni kushambulia kiini cha ukristo kama mtume Paulo alivyoandika

“Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tumemtumainia Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote” (1Wakorintho 15:17-19)

Maneno ya Paulo yana maana kubwa wapendwa. Kama Kristo hakufufuka, tumepoteza muda bure, kuomba kwa Mungu mfu, tumejinyima bure kwa ajili ya mtu aliyekufa miaka 2000 na zaidi iliyopita, na tumaini letu kuwa Yesu anatuandalia makao nayakuwa atakuja kutuchukua tena ni bure! Je waona sasa ni jinsi gani imani yetu inasimama au kuanguka katika kufufuka kwa Kristo? Naam, kama Kristo hakufufuka, ni heri tuishi na kuponda mali maana kufa kwaja!

Habari njema ni kuwa Kristo Yesu alifufuka katika wafu! Historia inashuhudia hivyo, na neno la Mungu linashuhudia hivyo. Wanahistoria kama Luka, Mathayo, Yohana, Josephus, Tacitus na wengine wengi wameandika mambo mbalimbali kuhusu kifo na kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo. Lakini hi ina maana gani kwetu? Kwa nini Yesu alikufa? Ni kwa ajili ya dhambi zetu! Unaweza sema utakwenda mbinguni kwa kuwa u mwema. Ndio, inawezekana u mwema ukilinganisha na Adolf Hitler. Lakini je Mungu anakuonaje? Mwema? Kama jibu ni ndio, hili ni jaribio waweza kufanya ili kujiona u mwema kiasi gani!

Hebu jiulize na iache dhamiri yako itoe jibu. Ulishawahi kusema uongo, hata mara moja katika maisha yako yote? Kama jibu ni ndiyo, wewe ni mwongo. Ulishawahi kuiba mali yoyote bila kujali thamani yake? Kama ndiyo, wewe ni mwizi. Ulishawahi kuzini? Hii ina maana hata kama ulimwangalia mtu ukamtamani, umezini naye moyoni mwako (Mathayo 5:27-28)? Kama ndio, wewe ni mzinzi. Umewahi kuua? Yesu alisema kumchukia nduguyo bila sababu ni kuua (Mathayo 5:21-22). Kama ndiyo wewe ni muuaji. Hivi ni vigezo vine kati ya kumi ambavyo Mungu atakuhukumu siku ya mwisho. Sikia Neno la Mungu linachosema:

“Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawaaturithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi , wala, wala watukanaji ”(1 Wakorintho 6:9-10)”.
Kwa kifupi, viwango vya Mungu viko juu sana, na wote tumetenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu (Warumi 3:23). Sote tumehukumiwa kwenda katika ziwa la moto, maana baada ya kifo hukumu (Waebrania 9:27). Mbele za Mungu Baba, aliye mtakatifu sana, hatufai na haki yetu itokanayo na matendo yetu ni kama takataka mbele za Mungu (Isaya 64:6). Mbele ya hakimu wa haki, hatuna la kujitetea. Tumetenda dhambi hali tukijua maana Mungu ameandika sheria yake katika mioyo yetu (Warumi 2:14-16). Kwa hiyo, kwa binadamu wote, ziwa la moto haliepukiki!

Habari njema ni kuwa, Yesu Kristo alikuja kulipa deni hili. Aliishi maisha Makamilifu ambayo mimi na wewe hatuwezi kuishi. Lakini pia alikufa, katika sehemu yetu, ili sisi tuishi. Kwa hiyo wote wanaokubali kazi yake msalabani na kufufuka kwake, wanahesabiwa haki, si kwa wema wao, bali kwa haki iliyo ndani ya Kristo Yesu (1Petro 3:18).

Mfano unaofanana kidogo ni huu, mko mbele ya mahakama, mnadaiwa deni kubwa sana ambalo hamwezi kulilipa. Hukumu imetolewa, mlipe deni au mwende kifungo cha maisha na viboko kila siku. Hamna uwezo wa kulipa na mnasubiri mpelekwe kifungoni. Ghafula hakimu anasimama na kusema, hizi hapa ni pesa toka mfukoni kwangu, nimelipa deni lote. Ila ili uhesabiwe umelipiwa sharti ukiri kwa kinywa na kuamini kwa moyo kuwa mimi hakimu nimekulipia deni lote. Hicho ndicho Yesu Kristo alifanya!

Bila ya Kristo, tunadaiwa, na mbele ya Mungu. Waanzilishi wa imani/dini nyingine zote hawakulipa deni la dhambi. Ni Yesu pekee alilipa. Mwamini Yesu Kristo leo upate kulipiwa deni lako na kuhesabiwa haki wewe ambaye bado hujampokea Yesu. Ni rahisi na haihitaji gharama. Ni lazima udhamilie moyoni kuacha dhambi na kuishi kwa ajili ya Kristo (Utubu). Biblia inasema ukimkiri Yesu kwa kinywa chako NA kuamini katika moyo wako kuwa Mungu alimfufua toka wafu UTAOKOKA. Chaguo ni lako!

Na wewe mpendwa ambaye umempokea Yesu Kristo, hili ndilo tumaini pekee ulilo nalo, ya kwamba Yesu alifufuka na anaandaa makao na atakuja kutuchukua muda wowote. Uwe tayari kwa siku hiyo(Yohana 14:2)

Neema ya Kristo na amani kutoka kwa NIKO iwe nanyi, Amina!

No comments:

Post a Comment