Wednesday, April 16, 2014

Historia Nyuma ya Utenzi wa Kaa Nami

“Kaa nami ni usiku sana, Usiniache gizani Bwana, Msaada wako Kwangu haukomi, Nili peke yangu Bwana Kaa nami” ni sehemu ya maneno ya wimbo huu unofikirisha na kutukumbusha kuwa tunapita tu hapa duniani na kuwa bila msaada wa Bwana Wetu, hatutashinda wala kufika mwisho kwa salama. Lakini ni nani aliuandika wimbo huu, na ni nini kilimsukuma kuandika maneno hayo?

 Sehemu ya Wimbo wa Kaa nami (Abide with me) ulivyoandikwa na mkono wa H.F. Lyte. Ukitaka nakala ya wimbo wote wasiliana nami!










Henry Francis Lyte alizaliwa mnamo tarehe 1 Juni mwaka 1793 akiwa sehemu ya familia ya Bwana Tomaso na Anna Maria Lyte huko Ednam, Uskochi. Tomaso baadaye aliamua kuitelekezafamilia na Anna akahamia mjini London, Uingereza na alifia huko, yeye na mwanawe mdogo. Akiviona vipawa vya Henry, Dkt. Robert Burrowes aliamua kumuasili na kumlipia ada na Henry akasoma Trinity College mjini Dublin huko Ireland akizama katika Ushairi.

Mwaka 1815 akaingizwa katika huduma ya kanisa La Uingereza (Anglican Church) na akatumikia parishi kadhaa huko Ireland na magharibi ya Uingereza. Miaka miwili baadae alikuwa ni kasisi wa Marazion, Cornwall, alipomwona na kumwoa Anne Maxwell, aliyekuwa na miaka 31 huku Henry akiwa na miaka 24 tu. Hata hivyo ndoa yao ilikuwa ya furaha na ulikuwa wakati mzuri wa Henry kusahau maumivu ya maisha yake.

Akiongea Kilatini, Kiyunani na Kifaransa, Henry alihamia mji wa wavuvi ulioitwa Brixham, mwaka 1824, na kanisa la Brixham lilikua kwa kasi baada ya kufika kwa Henry, kijana mtanashati, mshairi mzuri na mtu mwelewa wa mambo, mwanazuoni. Henry alihudumu kanisa hilo kwa miaka 23.

Imani ya Henry kwa kiasi kikubwa iliathiriwa na Abraham Swanne. Henry alikuwa akimhudumia Mchungaji Abraham, Jasiri mtu wa imani na asiyeogopa kifo. Mchungaji Abrahamu alikuwa akiuguzwa na Henry, akiwa katika hali ya kufa.

Akisumbuliwa na Mkamba na Pumu, na baadae Kifua kikuu, Henry alidhoofu sana. Hata hivyo alibaki kuwa mwenye furaha katikati ya dhiki hii.Mke wake Anna alijitahidi kutunza fedha na kuweza kumpeleka nchi za joto, Ufaransa na Italia wakati wa baridi.

Akiwa na miaka 54, akiwa amedhoofu, Henry alihubiri mahubiri yake ya mwisho. Katika mahubiri hayo ambapo aliwaaga watu wake na kuwakumbusha kuwa sote tutakufa na kuwa wale wote walioishika imani katika Kristo Yesu wamejiandaa vyema kabisa kukutana na kifo.

“Nasimama haba kati yenu leo, kama aliye hai toka kwa wafu, kama nitaweza kuliweka hili katika fikra zenu, na kuwafanya muwe tayari kwa saa ile kuu ambayo itawajia wote, kujitambulisha na kifo cha Kristo” . Baada ya ibada yake ya mwisho, Henry alikaa na kuandika mashairi ambayo leo tunayafahamu kama Utenzi uitwao “kaa nami”!

Wiki kumi baadae, Novemba 20, 1847, Franscis Henry Lyte alikwenda kupumzika kwa Baba Mbinguni. Utenzi wa kaa nami umekuwa ukiimbwa katika mashindano mbalimbali, ikiwamo kombe la Dunia kabla hawajauweka kando.

Bwana anatumia hata wadhaifu wa afya, kufanya mambo makubwa. Maisha ya Lyte yakutie moyo ufanye kazi ya Bwana bila visingizio



-Maranatha!

Vyanzo:
  1. http://www.poemhunter.com/henry-francis-lyte/
  2. Biography and hymns of Henry Francis Lyte (1793-1847), http://www.cyberhymnal.org/
  3. Dying Henry Lyte Asked God to Stay Near, http://www.christianity.com/church/church-history/timeline/1801-1900/dying-henry-lyte-asked-god-to-stay-near-11630479.html


No comments:

Post a Comment