Saturday, September 30, 2017

Siku Tutakapoimba HALELUYA!


Baada ya haya nikasikia sauti kama sauti ya umati mkubwa wa watu mbinguni ikisema kwa nguvu : “Haleluya! Wokovu na utukufu na uweza ni vya Mungu wetu, kwa maana hukumu Zake ni za kweli na za haki. Amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeuharibu ulimwengu kwa uzinzi wake. Mungu amemlipiza kisasi kwa ajili ya damu ya watumishi wake.’’

Wakasema tena kwa nguvu: “Haleluya! Moshi wake huyo kahaba unapanda juu
milele na milele.’’ Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti kuu: ‘‘Amen! Haleluya!’’

Kisha sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi, ikisema: ‘‘Msifuni Mungu wetu, ninyi watumishi wake wote, ninyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa!’’

Kisha nikasikia sauti kama sauti ya umati mkubwa wa watu, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi ikisema: ‘‘Haleluya! Kwa maana Bwana Mungu wetu Mwenyezi anamiliki. Tufurahi, tushangilie na kumpa utukufu!

Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo Imewadia, na bibi arusi wake amejiweka tayari.
Akapewa kitani safi, nyeupe inayong'aa ili avae.’’ (Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya
watakatifu.)
- Ufunuo 19: 1 – 8

1. MAANA YA NENO HALELUYA
Kwa baadhi ya watu Neno Haleluya ni moja ya maarufu sana katika kujaribia kipaza sauti. Ikikolezwa na “Bwana Yesu Asifiwe” basi inafaa sana kwa kujaribia kama mitambo ya sauti imekaa sawa. Kwa wengine ni sehemu ya kuwalazimisha “walokole wenye masikio ya utafiti” wawasaidie katika kupata umaarufu wao. Na kwa wengine ni neno ambalo kama maneno ya kuimba yamewaishia basi ndio neno sahihi la kurefusha wimbo ili kumalizia dakika walizopewa kuimba.

Kuna ufahamu anuai juu ya neno Haleluya ambao wakati mwingine umeleta makwazo na maumivu, huku wakati mwingine ukiwapa wengine “hatua” ambazo wako tayari kuzipata kwa gharama yeyote. Vyovyote iwavyo neno Haleluya lina asili na maana yake halisi. Swali la msingi hapa si kama Haleluya inasemwa na kuimbwa namna gani bali ni nini maana ya neno hili na nani haswa anapaswa kulisema ama kuliimba!

Katika agano la Kale, ambalo kwa sehemu kubwa limeandikwa Kiebrania, neno Haleluya ni mkusanyiko wa maneno mawili “Hallelu” lenye maana “(Ninyi) msifuni” na “Yah” lenye kubeba Jina la Mungu wa Israeli, yaani Yahwe. Kwa hiyo katika matumizi yake katika agano hilo (na Biblia kwa ujumla) ina maana Msifuni (ninyi) Yahwe ikiwa ni neno ambalo linatoa amri (imperative). Katika Agano Jipya ambalo limeandikwa kwa Kiyunani, Neno hili “Alleluia” lina maana sawa na ile ya Kiebrania.


2. UZITO WA NENO HALELUYA
Wengi wamelitumia neno Haleluya vibaya. Hii ni kwa sababu ya Ujinga wa maana na uzito halisi wa neno hili. Haleluya ni Neno alilolichagua Mungu aliyeumba mbingu na dunia kama neno la amri kwa ajili ya sifa na utukufu wake. Huyu si mungu kama ilivyo miungu ya dunia hii isiyo na idadi, bali ni Mungu ambaye Uweza wote na Utukufu ni wake peke yake. Ni Mungu ambaye Hukumu zake ni za haki.

Ni Mungu aliyeona maovu ya dunia nyakati za Nuhu na akaangamiza “Kila kitu chenye uhai juu ya uso wa nchi kilifutiliwa mbali, watu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege warukao angani wakafutiliwa mbali toka duniani” (Mwanzo 7:23). Ni yule ambaye aliangamiza miji ya Sodoma na Gomora na hata leo tuna ushahidi wake. Si Mungu ambaye unaweza mchezea wala kumtetea. Yeye ndiye Mungu mkuu, Muumba na Mmiliki wa vyote ikiwemo nyumba yako, ukoo wako, mali zako na uhai wako.

Hukumu za Mungu wetu ni za Haki na hapepesi macho wala kufumbia macho uovu wowote. Kama alivyoihukumu dunia ya enzi za Nuhu ndivyo atakavyomhukumu kila mmoja wetu kwa kuvunja sheria yake. Kwa wizi uwe “mdogo” wa kalamu au “mkubwa” wa ujambazi, tamaa ya macho, ulevi, uzinzi na kila ambalo Yeye kama mmiliki halali wa wanadamu wote ametukataza tusifanye. Yeye ni Yah katika Haleluya ambaye hatupaswi kulitaja jina lake bure kama sehemu ya kutafutia umaarufu, kujaribia vipaza au namna yeyote ya kulishusha jina lake. Jina lake ni kuu sana na lafaa kuheshimiwa na kila kitu na kila mtu.

Kwa hiyo Neno Haleluya linapaswa kutamkwa tu pale ambapo tunamsifu Mungu aliye hai na si vinginevyo. Kumbuka Neno hili limebeba Jina Takatifu sana la Mungu ambaye alisema wazi bila kificho “Usilitaje jina la BWANA Mungu wako bure, kwa kuwa BWANA hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure” (Kumb 5:11). Kwa hiyo ni kosa kubwa kulitumia Jina la Mungu Muumba wa Mbingu na nchi, ambaye uhai wako uko mikononi mwake, naye utakutana nae nukta moja baada ya kifo chako. Ni hatari sana, na ni upumbavu mkuu kujitia katika hatari hii.

3. HAKI YA KULITUMIA NENO HALELUYA
Kutokana na asili na maana ya neno Haleluya, sio kila mtu ana haki ya kulitamka. Biblia imeweka wazi kuwa ‘‘Msifuni Mungu wetu, ninyi watumishi wake wote, ninyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa!’’ (Ufu 19:5). Ni watumishi wa Mungu pekee, wakubwa kwa wadogo wanaopaswa na kuruhusiwa kulitamka hili neno bila hofu ya kujiletea hatia juu ya vichwa vyao. Hii ni kwa sababu watumishi wa Mungu aliye hai ni sehemu ya Kanisa, yaani Bibi-Harusi wa Kristo ambaye ameandaliwa karamu kuu mbinguni ilhali wengine wote sehemu yao ni katika ziwa la moto.

“Kisha nikaona kiti kikubwa cha enzi cheupe, dunia na mbingu zikaukimbia uso wake Yeye aliyeketi juu yake, wala mahali pao hapakuonekana. Nami nikawaona wafu wakubwa na wadogo, wakiwa wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi na vitabu vikafunguliwa. Pia kitabu kingine kikafunguliwa ambacho ni cha uzima. Hao wafu wakahukumiwa sawasawa na matendo yao kama yaliyoandikwa ndani ya hivyo vitabu... Iwapo mtu jina lake halikuonekana katika kile kitabu cha uzima, alitupwa ndani ya lile ziwa la moto. (Ufu 20:11-15)

Kama wewe si sehemu ya Watumishi wa Mungu, basi ujue sehemu yako ni Jehanamu iwakayo moto. Je, utapata faida gani kufurahia maisha ya dhambi miaka hata mia, kama Mungu atakupa kuifikia na kisha baada ya hapo kupotelea kwenye maumivu milele? Kwa nini upotelee “Mahali ambako ‘funza wake hawafi, wala moto hauzimiki’”?

Jehanamu ipo, na wanaokwenda huko wapo (na wengine walishafika). Je huoni kama ni wakati wa kutafakari kama kweli umekubali kwa moyo wako wote kuishia motoni milele?
Pengine unajisemea kuwa huu ni upuuzi! Kama ndivyo, Neno la Mungu lina habari njema nawe. Linakwambia hivi: “Atendaye mabaya na aendelee kutenda mabaya, aliye mchafu na aendelee kuwa mchafu...” (Ufu 22:11). Kwa maana nyingine ni kuwa endelea kuponda maisha Jehanamu ya moto inakusubiria, na wakati wako utafika wala hakutakuwa na wa kukuokoa!

Kwako wewe ambaye unaona huwezi kukubali kwenda Jehanamu nina habari mbaya na kisha njema. Habari mbaya ni kuwa tayari uko njiani kwenda Jehanamu na Mungu akiamua wakati wowote kuondoa pumzi yake ya uhai aliyokupa, utaamkia kuzimu kusubiria hukumu yako ya mwisho, yaani Jehanamu ya Moto. Hauna jinsi ya kujisaidia na deni la kuvunja amri ya Mungu hauwezi kulilipa milele yote.

Habari njema ni kuwa hauna ulazima wa kulilipa wewe. Mungu katika huruma na rehema zake, aliamua kuibeba hukumu ya hatia yako yote. Katika kulitimiza hilo aliamua kuongeza uanadamu katika Uungu wake na akakaa nasi katika Utu wa Yesu Kristo. Akaishi miaka 33 bila kutenda dhambi yoyote na hivyo hakustahili kufa, maana mshahara wa dhambi ni mauti. Lakini kwa kukupenda wewe akaamua kufa akibeba adhabu uliyoistahili ili wewe uwe na Uzima alioustahili, tena uzima wa milele.

Kwa kuwa Alikuwa (na hata leo ni) Mungu, aliweza kubeba adhabu ya dunia nzima kwa kipindi kile. Kisha akazikwa na siku ya tatu akafufuka akitangaza ushindi juu ya kifo na mauti.

Deni hilo halilipwi tu kiautomatiki. Malipo yanamhusu kila anayekiri kuwa Yesu ni Bwana Mungu wake na kuwa Mungu Baba alimfufua toka kwa Wafu, na kisha kuamua kuacha njia za dhambi na kumlilia Yesu amuokoe. Basi kwake huyo deni lake litasamehewa na Jina lake litaandikwa katika kitabu cha Uzima.

Huna muda wa kupoteza kama unazitaka rehema za Mungu kabla hujachelewa. Hapo ulipo omba toba na rehema toka kwa Mungu wako aliyekuumba, Yesu Kristo. Hakuna namna nyingine ya kuepuka Jehanamu ya moto isipokuwa hii tu. Ni njia pekee ya kukufanya uwe sehemu ya Kanisa, yaani Bibi harusi wa Kristo, na kuwa na uhakika wa kuwepo katika sherehe kubwa sana ijayo huko Mbinguni. Huko tutaimba Haleluya kwa Mungu wetu, na kwa Mwanakondoo wa Mungu aliyekufa kwa mateso ili atuokoe na Jehanamu!

Naam! Utakuwa sehemu ya kile Mtume Yohana alichokisikia kuwa kuwa ni “sauti kama sauti ya umati mkubwa wa watu, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi ikisema: ‘‘Haleluya! Kwa maana Bwana Mungu wetu Mwenyezi anamiliki. Tufurahi, tushangilie na kumpa utukufu!

Na haitakuhitaji usubiri kufika Mbinguni ndipo uimbe haleluya, kwa sababu Bwana atakusamehe dhambi zako zote, nawe utaimba “Haleluya, wewe ni Mungu Mwokozi”. Na tena Bwana atakuongoza na kukufundisha njia ya kuiendea nawe Utasema, “Haleluya, Bwana unastahili!”. Na Yote katika Yote utagundua kuwa na utatamani kuwaambia wengine Hallelu-Yah, yaani msifuni ninyi Bwana Mungu wetu

.... Haleluya, Amen!