Tuesday, May 20, 2014

Siku Utakapovuta Pumzi yako ya Mwisho

Jabu alikuwa anatembea barabarani kwenda kumwona mkewe. Mkewe alikuwa na malaria na alikuwa amepumzishwa katika zahanati ya mtaa wao. Akiwa anavuka barabara ya mwisho kabla ya kuifikia zahanati, ghafla anasikia watu wakipiga kelele za uoga. Alipogeuka akaona lori la mizigo limeacha barabara likimfuata. “mamaaa!” akapiga kelele ukijaribu kulikwepa. Kitu cha mwisho anachokumbuka ni kishindo kikubwa na maumivu makali.

Baada ya hapo alijihisi kama anajivua toka katika mwili, mithili ya nyoka anayejivua gamba. Ghafla akawa kama anazama katika giza kubwa na macho yake yakififia mithili ya taa hafifu katika ukungumzito. Sambamba na hilo alianza kuhisi joto likiongezeka na kuwa kali na harufu mbaya ya moshi wa yai lililooza ukiibuka. Kwa sabau alikuwa mtaalam wa kemia, Jabu alijua ni salfa inayoungua. Hakuweza kupumua vizuri kabisa kwa moshi mzito na harufu kali. Hofu kuu ilimshika, na hakuelewa ch kufanya. Kufumba na kufumbua, Jabu alikuwa katika eneo kubwa ambalo hakuweza kujua limeanzia wapi wala kuishia wapi. Alichoona ni moshi mzito na giza nene. Alichosikia ni sauti nyingi sana zikilia kwa maumivu makali. Hakujua kama alikuwa analia au anagugumia, lakini alijua kwa hakika alikuwa akisaga meno kwa maumivu makali aliyoyasikia.

Jabu alikumbuka siku moja kanisani ambapo mchungaji wake elielezea sehemu inayoitwa kuzimu, ambayo inafanana na hapa alipo. “hapana, sio kwamba panafanana, ndio penyewe!” alijisemea moyoni. Jabu alianza kujilaumu kwa nafasi zote alizozipoteza. Akakumbuka watu waliomsihi kwa machozi na kumwonyesha njia impasayo, lakini aliwadharau na kuwapuuza. Sasa alikuwa katika mahali alipodhani hapakuwahi kuwepo, na alijua hakuna jinsi ya yeye kutoka. Alitamani iwe ndoto, lakini haikuwa hivyo.

Aliwashukuru wale watu walioonekana vichaa njiani wakidharauliwa,kwa upendo wao. Moyo wake ulimuuma sana. Akamkumbua rafiki yae Mwema, aliyekuwa akienda kanisani kila siku na hakuchukua muda kumuonya. “Pengine angesema kwa kuwa ni rafiki yangu ningemsikia”. Namchukia kwa alilolifanya. Alitamani arudi akawonye rafiki zake kuwa kuzimu ipo, na sio mahali pa kwenda, lakini hakuwa na namna. Kifo kilikuwa kimemtenga na mahali pa walio hai, tumaini na wema vimemwacha. Aliungana na aliowakuta huko kulia kilio cha kukata tamaa......!

Kuzimu na Jehanamu Ipo
Watu wengi wanadhani hii ni hadithi ya kufurahisha kama ilivyo hekaya za abunuwasi au alfu lela-ulela. Shetani, adui wa roho yako anajua pia kama ataifanya Jehanamu na Ziwa la mot vionekane ni visasili, atakufanya uvipuuze. Lakini hebu jiulize: unawekeza nguvu na raslimali zako kiasi gani kuhakikisha unaishi maisha mazuri hapa duniani? Umesoma vitabu vingapi vya “jinsi ya kufanikiwa” au vifananvyo na hivyo? Mara ngapi umefanya hili na lile kuhakikisha unafanikiwa? Au ni miaka mingapi umekuwa shuleni lengo likiwa ni ufanikiwe? Halafu jiulize umetumia raslimali kiasi gani kujua utakakokwenda baada ya miaka michache sana uliyo nayo? Utagundua unatania!

Neno la Mungu lipo wazi kuwa baada ya kifo ni hukumu (Waeb 9:27). Ukifa faili la maisha yako linakuwa limefungwa na mahali pa kwenda pameamuliwa. Mungu aliyeumba mbingu na nchi, aliweka utaratibu wa sisi kuishi katika dunia yake (Kutoka 20:3-17). Alikataza watu kusema uongo, kuiba, kuwa na miungu, katika dunia yake. Na aliweka adhabu kwa wavunjaji wote, nayo ni Ziwa la moto (Ufun 21:8, 1 Kor 6:9). Baada ya kufa nafsi yako itakwenda “selo” kusubiri siku ya kusomewa hukumu yako. Huko ndiko kuzimu ambako hakuna raha bali ni maumivu (Luke 16:22-24). Utakuwa ukijielewa na maumivu utayasikia. Hili ni tone tu ukilinganisha na hukumu yenyewe.

Neno liko wazi kabisa kuwa iko siku Mungu ameiandaa kwa ushahidi kabisa (tazama somo hili kwa makala inayohusiha hilo). Wengi wanadhani Mungu ni kama mjomba Santa, akileta zawadi za Krismasi. Lakini kwa kweli wengi watapigwa namshangao watakapokutana uso kwa uso na Muumba wao. Mungu anatisha kwa kuwa ni mkuu mno. Yeye Mungu “ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. ” (1Tim 6:16). Mpendwa wangu, Mungu sio yule uliyedanganywa. Na kwa hasira yake aliiandaa Jehanamu ya moto kwa shetani na wote watakaomfuata katika uasi wa sheria ya Mungu.

Baada ya Mungu wa haki kukuonyesha yote uliyofanya na jinsi bila soni ulivyovunja amri zake atakuhukumu kwenda katika ziwa la moto. Wewe na selo mtatupwa katika gereza la mwisho, yaani Ziwa la moto (Ufun 20:14-15). Hapo ni kilio na kusaga meno milele maana huko “funza wao hafi, wala moto hauzimiki” (Mark 9:46, Luk 13:28).

Jehanamu siyo sehemu ya kwenda mpendwa, na Mungu siyo wa kukutana naye kama jaji, maana anatisha. Yesu mwenyewe alionya kuwa kama “mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum” (Mark 9:45). Jehanamu ni mahali pabaya kiasi kwamba nakushauri kama gari lako, mke, mume au chochote kitakuwa sababu ya wewe kwenda huko kitupe.

Yawezekana umeashaanza “kutenda mema” ili upate sababu ya Mungu kukuruhusu uende mbinguni. Nikuhakikishie hata utende mema kiasi gani hayafuti makosa uliyofanya, na kujaribu kumhonga Mungu matendo yako ili “asahau” makosa yako ni kosa kubwa zaidi. Mungu anayaita matendo yako hayo kuwa ni kama “nguo iliyotiwa unajisi” (Isay 64:6). Usijaribu kumpa Mungu rushwa ya matendo mema, hataipokea! Na usijidanganye kwamba Mungu atakusamehe”ukitubu”. Jaribu kumwambia hakimu nimeiba ila ninatubu, nisamehe uone. Kama mwanadamu anasimamia sheria za wanadamu vema, unadhani Mungu si zaidi kusimamia sheria zake mwenyewe?

Waweza kuwa unajiuliza kuwa “kama ni hivyo nifanye nini sasa ili nami niiepuke Jehanamu?” Jibu ni kuwa huna cha kufanya. Mungu alifanya mwenyewe. Mungu alitwaa mwili akakaa kwetu (Yoh 1:14) akaishi maisha matakatifu na kufa kwa ajili yetu, akilipa deni la hatia yetu: ili sisi tulio wa dhambi na tuliohukumiwa Jehanamu tupate kwenda Mbinguni. Yesu alilipa deni la dhambi zote hivyo hakuna sababu ya wewe kwenda Jehanamu. Unachopaswa kufanya ili deni la uasi wako lifutwe ni kumkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa alikufa kwa makosa yako na kuomba akusamehe na kukuosha dhambi zako, utaokoka!

Pamoja na kuwa Mungu amelipa, kuna watu watakwenda huko kwa sababu ya kiburi. Ukikataa neema ya Mungu leo utajutia siku moja. Na siku hiyo yaweza kuwa hata leo. Je wajua kitakachofuata dakika tatu zijazo? Usiwe mpumbavu kama Jabu, kupoteza nafasi hii adimu.mkiri Yesu leo akuokoe na adhabu kali ya Mungu wa Mbinguni.

Bwana Yesu na akubariki,
Maranatha!

Saturday, May 3, 2014

Swali #1 – Je Daniel Alikosea Jina la mfalme wa Mwisho wa Babeli?


Swali
Danieli Sura ya Tano inasema Belshaza ndiye alikuwa mfalme wa mwisho wa Wakaldayo. “Usiku huo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa. Na Dario, Mmedi, akaupokea ufalme, naye umri wake alikuwa na miaka sitini na miwili.” (Dan 5:30-31). Katika maandishi ya wanahistoria wengine haiko hivyo na kutoka katika maandiko ya kale tunajua kuwa Nabonidus ndiye alikuwa mfalme wa mwisho wa Babeli kabla ya uvamizi wa Wamedi na Waajemi uliopelekea mwisho wa dola ya Wakaldayo. Kama Daniel alikuwepo enzi hizo aliwezaje kukosea kitu kilicho wazi hivi? Na kama alikosea jambo rahisi kama hili tutaaminije kama kitabu hiki sio utunzi wa Mtu fulani baada ya matukio (ambapo ni rahisi kukosea kwa kuwa hakuwepo)?

Jibu
Danieli ni moja ya vitabu vya Biblia ambavyo vimeshambuliwa sana, na kwa sababu ambayo mtu yeyote aliyeyasoma haya au kuyatafiti atayaelewa. Wenye kushuku na wasioamini Biblia hawana jinsi ya kutimiza malengo yao bila kushambulia vitabu hivi kwa kuwa vimejaa uthibitisho kuwa Biblia haiwezi kuwa Neno la mwanadamu kwa kuwa imetabiri kwa kina matukio, na mambo na falme kwa usahihi kiasi kwamba hakuna namna mwanadamu angeweza kuandika. Moja ya vitabu vya Biblia vyenye unabii huu wa kutisha ni kitabu cha Daniel.

Mashambulizi hayakuanza jana wala juzi. Polfili, mwanafalsafa wa kipagani ni moja kati ya watu wa mwanzo kabisa kukishambulia kitabu hiki. Hatujabakiwa na kazi zake ila tunaweza kujua kupitia wanatheolojia waliokuwa wakijibu mashambulizi haya. Mathalani, Jerome katika maoni yake juu ya kitabu cha Danieli anasema

Polfili aliandika katika kitabu chake cha kumi na mbili dhidi ya unabii wa Danieli, akikana kwamba kiliandikwa na mtu ambaye kitabu hiki kimepewa jina lake, ila mtu mwingine aliyeishi Yudea wakati wa Antiokasi aliyeitwa Epifania. Na zaidi ya hayo anadai kuwa “Danieli” hakutoa unabii juu ya wakati ujao kama ambavyo alisema juu ya wakati uliopita, na mwisho kuwa chochote alichosema mpaka wakati wa Antiokasi kilikuwa ni historia thabiti, wakati chochote alichojaribu kubahatisha zaidi ya wakati ule kilikuwa si kweli, kama ambavyo asingeweza kujua wakati ujao

Mashambulizi ya leo juu ya kitabu hiki aidha ni marudio ya mwanafalsafa huyu, yakiwa yamepakwa rangi ya ukisasa au ni mapya yakifuata msingi wa Polfili. Kitu kimoja ambacho kilimfanya huyu mwanafalsafa afikie hitimisho lake hili ni kuwa maandiko katika Danieli yalitimia hata nukta. Kwa akili timamu ya kawaida kabisa, hakuna namna Danieli angeweza kujua mambo yajayo kwa usahihi hivyo: alijua haukuwa ubahatishaji. Kwa hiyo alibakiwa na njia mbili za kufuata. Aidha Daniel aliandika karne ya 6 K.K au atengeneze namna ya maelezo kuwa ni uhuni uliofanywa baada ya matukio. Bahati mbaya alichagua njia ya pili ambayo siyo ya kweli.

Nikirudi kwenye swali la leo ambalo wengi wa wanaolitumia kama ngao ya kukwepa kuiamini Biblia hufuata nyayo za Polfili, limetokana na kutokuelewa historia na kutojishughulisha. Japo wengi wamelikimbia swali hili na hawalitumii tena, bado wapo wenye kushuku wanaolitumia ili pengine kuwapotosha Wakristo wachanga na wengine wasiojua. Mfano katika maandiko yao, “Skeptic Annotated Bible” wameandika “mfalme wa mwisho wa Babeli alikuwa Nabonidasi aliyetawala toka 556 mpaka 539 and aliyeshindwa na Koreshi. Alikuwa Nabonidasi na si Belshaza aliyekuwa wa mwisho katika wafalme wa Babeli.”

Kwanza hatutumii historia kujaribu kuhukumu Neno la Mungu. Wanahistoria nje ya Biblia wamekuwa wakikosea mambo mengi na hata majina mbalimbali, na unapofanyika ugunduzi wa mambo ya kale, Biblia imekuwa ikithibitishwa kuwa sahihi. Hata hivyo, kwa hili historia ya nje ya Biblia iko sahihi, na Biblia haijakosea. Mfalme wa mwisho wa Babeli hakuwa Belshaza bali Nabodinasi. Na ndio maana Biblia inasema yafuatayo baada ya Danieli kutafsiri maneno yaliyoandikwa na kiganja mbele ya Belshaza:

Ndipo Belshaza akatoa amri, nao wakamvika Danieli mavazi ya rangi ya zambarau, wakatia mkufu wa dhahabu shingoni mwake, wakapiga mbiu kutangaza habari zake, ya kwamba yeye ni mtu wa tatu katika ufalme. (Danieli 5:29)

Hapa Daniel anapaswa kuwa mtu wa tatu kwa kuwa tayari Belshaza alikuwa ni mtu wa pili na kwa hiyo alikuwepo mtu wa kwanza, naam, naye ni mfalme Nabodinasi. Katika andiko la Nabonidus mwenyewe linalofahamika kama "Nyakati za Nabodinasi"[1] tunajua kuwa "Mfalme alitumia miaka kumi huko Araba na akaacha Babeli ikisimamiwa na mwana wake Bel-Shar-Usur [Belshaza]". Kwa hiyo wakati nabonidasi hakuwepo Mfalme wa Babeli alikuwa Belshaza lakini akiwa mtu wa pili na si wa kwanza. Kwa hiyo Biblia hapa ipo sahihi kwa kuwa Danieli, aliyeandika kitabu hiki alishuhudia aliyoyaona.

Kuna Jambo kubwa zaidi ya hili la Danieli kuwa sahihi. Nalo ni kuwa Mungu aliyesema na Danieli, Yeye aliyeumba mbingu na nchi, ametenga siku awahukumu wanadamu wote sawasawa na matendo yao. Mungu atatuhukumu si kwa matendo tu yaliyo maovu bali hata mawazo na nia ovu zote. Siku hii ya kutisha inakuja na njia pekee ya kuepuka hukumu hii ni kujisalimisha kwa Yesu Kristo, yeye aliye mwokozi wa wanadamu wote. Leo hii umlilie yeye, utubu na kugeuka toka njia zako mbaya. Naye atakusamehe makosa yako na kukupa uzima wa milele. Kumbuka Yesu anakuja, furaha kwa watu wake na huzuni, kilio na kusaga meno kwa waliomkataa.

Maranatha!

[1] http://www.britishmuseum.org/explore/highlights/highlight_objects/me/c/cuneiform_fall_of_a_dynasty.aspx