Wednesday, January 11, 2017

Swali #3 - Je Kuna uhusiano kati ya sayansi na Mungu?

Swali hili limeulizwa na msomaji wetu likiwa na sehemu mbili ambazo zinafanana:
  1. Je kuna uhusiano kati ya Mungu na Sayansi?
  2. Je Ukweli ni upi kati ya binadamu alikuwa nyani na kutoka kwa Adamu na Eva?
Jibu: 
Ni vema kabla ya kujibu haya tukaweka sawa tafsiri za maneno ili  yanapotamkwa wote tuwe na uelewa mmoja wa maneno hayo.  Sayansi imetokana na neno la  Kilatini "scire" lenye maana Fahamu. Mnyumbulisho wake, yaani "scientia" (ufahamu) ndilo limezaa neno sayansi. Kifupi Sayansi maana yake ni ufahamu. Mungu, kwa upande mwingine ni Yeye aliye mkuu kuliko wote, asiye na mwanzo bali Mwanzo wa vyote na asiye na mwisho ila ni Mwisho wa vyote. Hii ni tafsiri fupi ambayo haisemi kila kitu kuhusu Mungu, lakini inatosha kwa mada yetu hii. Kwa hiyo kimsingi swali la msomaji wetu ni kuwa "Je kulingana na ufahamu tulionao (sayansi) je kuna Mungu aliyeumba Adam na Hawa au tulibadilika toka viumbe wengine"? Jibu nitalitoa hapo chini, kwa sasa tuangalie pande mbili za Swali.

1. Je Kuna Tunafahamu kuwa kuna Mungu? Kama Yupo, Anahusianaje na Sayansi?
Hili ni swali la msingi ili kabla ya sehemu ya Pili. Biblia inatuambia "hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi" (Mwa 1:1) na Tena inatuambia Warumi 1:20 inatuambia kuwa sote tunajua ya kuwa Mungu yupo na hatuna udhuru.

 "Kwa sababu mambo yake [Mungu] yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru
- Warumi 1:20 (msisitizo ni wangu)

Kama ni kweli basi yapaswa kuwepo na mambo yanayoonyesha wazi kuwa kuna Mungu. Yafuatayo ni Mambo mawili kati ya mengi sana, ambayo yanathibitisha ukweli wa andiko hili na kuonesha uhusiano wa sayansi na Mungu. Kumbuka, hivi si vipimo vya uwepo wa Mungu, bali ni alama (fingerprint) alizoacha makusudi ili kila anayemtafuta ajue Yupo!

i. KANUNI YA ULINGANIFU, SAYANSI NA MUNGU
Ili sayansi iweze kufanya kazi lazima kuwe na ulinganifu (uniformity). Sayansi kamwe haiwezekani kama vitu vinakwenda ovyo ovyo. Mfano huu utakuonesha mazingira ambayo hakuna ulinganifu. "Gari lilikuwa inakwenda 100km/saa kwa saa kisha bila kuguswa wala mazingira kubadilika likaanza kurudi kinyume nyume kwa 120km/saa halafu ghafla likapaa na halikurudi tena". Unaweza kucheka lakini huu ndio ukweli, bila ulinganifu hakuna sayansi maana inawezekana leo unachanganya kemikali A na B zinatoa C na kesho unachanganya kemikali A na B katika mazingira yaleyale unapata X. Ili Sayansi iwezekane inahitaji kuwe na ulinganifu.

Swali la msingi linakuja hapa: Kwa nini kuna ulinganifu na si shaghala bhagala? Je ni nani/nini aliyeweka kanuni ya ulinganifu na kuisimamia? Biblia ipo wazi kuwa ni Mungu ambaye anavishikilia vitu pamoja na ameamuru viende kwa ulinganifu.

"Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma."
- Mwanzo 8 : 22

Hapa tunaona kwamba ni Mungu mwenyewe ndiye aliyeamuru kuwe na ulinganifu. Tuna uhakika mwakani kutakuwa na masika tena kwa sababu Mungu alituahidi itakuwa hivyo. Lakini si hivyo tu. Mungu ndiye anayashikilia mambo yote ili yakapate kuwa na ulinganifu. Biblia tena inatuambia:

" ... akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake (upholding all things by the Word of His power)" - Ebr 1:3

Je kuna Mungu? Jibu ni ndio. Ulinganifu tunaouona hauwezekani kama hakuna Mungu. Vinginevyo lazima ueleze ni kwa nini vitu vina ulinganifu badala ya shaghala bhagala. Je kuna uhusiano wa Sayansi na Mungu? Ndio! Mungu anaweka sheria za msingi za Sayansi na kufanya tuwe na uwezo wa kujua mambo yote tunayojua. Hapa nimejadili kanuni/sheria moja tu. Mungu akitupa Neema basi tutajadili nyingine.

ii. TUNAJUAJE TUNAYOJUA KUHUSU TUNAVYOVIJUA?
Ulishawahi kujiuliza hili swali? Mara nyingi tunaongea mambo na kudhania tunajua. Lakini huwa hatujiulizi swali, tunajuaje? Mfano ni mtu anaposema "haki haikutendeka". Anajuaje kilicho haki na kuwa haikutendeka? Haki sio kitu kama nyanya ambacho unaweza kukiona au kukigusa. Mfano mwingine ni hesabu. Hatuwezi kugusa hesabu wala kuziona. Lakini huwa"tunajua" hesabu. Mifano ipo mingi ila swali la msingi ni kuwa tunajuaje tunavyojua?

Kila mtu ana mtazamo ambao kimsingi ni namna anavyotafsiri matukio mbalimbali ya dunia hii. Mtazamo unajengwa na vitu ambavyo huwezi kuvithibitisha, ila unaamini ni kweli. Kwa maana nyingine, mitazamo yote imejengwa kwa kuamini. Kwa mfano, wote tunakubali kuwa lazima tuwe na uongozi, na kwa hakika tuna viongozi. Lakini ni kwa nini lazima tuwe na viongozi? Unaweza kutaja faida za kuwa na viongozi. Hii haitoshi kwa sababu kuna hasara pia za kuwa na viongozi. Na zaidi faida za uongozi sio sababu ya ulazima wa kuwa na uongozi. Hii ni sehemu ambapo mtazamo wa mtu unaingia.

Watu wanaweza kuwa na ushahidi uleule lakini jinsi watakavyoutafsiri itategemeana na mtazamo wao juu ya dunia. Dunia tuliyo nayo ni ileile. Ila kuna wanaosema imekuwapo kwa maelfu ya miaka na wengine wanasema imekuwapo kwa mamilioni ya miaka. Mtazamo ni kama lensi za miwani. Mtu aliyevaa miwani yenye lensi nyekundu, ataona vitu kwa rangi isiyo sawa na aliyevaa myeupe au ya kijani. Vitu vyeupe ataviona ni vyekundu.

Mtazamo ni mada inayojitegemea, ila kwa sasa itoshe kukupa mwanga. Tukirudi katika mada husika, kuna mitazamo miwili. Hii si mitazamo pekee, ila ni mitazamo inayotawala katika mada ya Mungu na sayansi. Mtazamo wa kwanza ni ule wa nadharia ya mageuko (evolution theory) na ule wa Uumbaji (creationism). Hebu tuangalie kwa ufupi misingi ya mitazamo hii.

Nadharia ya mageuko inasema hivi. Kulikuwa na nukta moja iliyokuwa imegandamizwa sana. nishati, maada na nafasi vyote vilikuwa katika nukta hii. Kisha ukatokea mpasuko mkubwa, ile nukta ilipasuka; Na katika mpasuko huo mabonge ya moto yalisambaa, miaka yapata bilioni 13.4 iliyopita. Kwa miaka milioni nyingi, mabonge haya yaliendelea kupoa na baada ya muda, katika moja ya bonge hilo kulianza kunyesha mvua na kutengeneza bwawa la kemikali mbalimbali. Kwa miaka mamilioni ya mchanganyiko katika "supu" hii, kukatokea kiumbe hai cha seli moja. Kufanya hadithi iwe fupi seli hii moja ilipitia hatua za mageuko kwa mamilioni ya miaka na kutoa aina mbalimbali ya viumbe hai tuvionavyo leo. Hakuna Muumbaji kwa watu wa mtazamo huu na vitu vyote ni sawa. Hakuna tofauti ya wewe na ndege kwale kiuhalisia. Wote ni wanyama tu.

Kwa upande mwingine, wale wa upande wa Uumbaji, wao wanaamini kuwa hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi na vyote vilivyomo (Mwa 1:1). Kwamba kumekuwa na mabadiliko ndani ya aina za wanyama. Mbuzi ameendelea kubadilika kuwa mbuzi na mbwa akiwa mbwa. Mbwa mkubwa, Mbwa mwitu ... lakini ni mbwa. Hakuna mageuko ya kutoka aina moja kwenda nyingine, katika mtazamo huu. Mwanadamu ameumbwa maalum kwa mfano wa Mungu na hivyo ni tofauti na viumbe wengine wa Mungu duniani.

Sasa tukirudi kwenye swali la msingi, tunajuaje tunavyojua? Kwa upande wa mtazamo wa mageuko hakuna namna ya kujua. Kwa ukweli kabisa hakuna kujua wala kutojua. Kama sisi ni matokeo ya muunganiko wa kemikali, basi mwanadamu si zaidi ya kemikali. Kinachoendelea katika ubongo wangu ni mipambano ya kemikali na kama mipambano hiyo itaamua kuwa 2+2=3 hakuna tatizo kwa sababu kemikali katika ubongo wako zaweza kuamua 2+2=6. Kama ubongo ni mpambano wa kemikali na umeme basi hakuna anayekosea. Lakini tunajua kuwa kuna kujua na kutojua na kuna ukweli na uongo. Kwa hiyo nadharia si sahihi na imeshindwa kueleza kwa nini tunajua tunavyojua.

Kwa upande wa Uumbaji hili ni suala rahisi. Mwanadamu ni nafsi hai (Mwa 2:7) ambaye ameumbwa kwa mfano wa Mungu (Mwa 1:26-27). Kwa hiyo Mungu ameweka katika mwanadamu uwezo wa kuwaza, na kuwa na utashi wa kuamua. Mwanadamu sio kemikali za Ubongo tu bali kuna sehemu ambayo haionekani kwa macho. Kwa sababu hiyo kuna kujua na kutojua, uongo na ukweli. Mungu ndiye anayesema kipi ni kweli na kipi ni uongo, na ndiye Mkuu katika yote.

JUMLA YA YOTE
Mada hii ni pana sana, na hapa nimegusa chembe tu, nikigusa sehemu chache kwa kifupi sana. Kwa kukazia niliyokwisha kuyasema ni kuwa, uhusiano wa Mungu na sayansi ni kuwa Mungu ndiye muumbaji wa vyote. Ndiye aliyeweka sheria/kanuni zinazosimamia maumbile na uumbaji ambazo sisi tunatafuta kuvijua. Sayansi ni kujua yale ambayo Mungu ameyaweka. Hakuna ushahidi uwao wowote wa kuonyesha ukweli wa nadharia ya mageuko. Na kwa sababu nadharia hii imekuwa mtazamo kwa wengi basi kila ushahidi wanautafsiri kwa lensi za mageuko.

Hakuna mgongano kati ya Mungu, Neno lake (Biblia) na Sayansi.

NUKUU ZA ZIADA
Hawa ni wanasayansi wachache walioamini uwepo wa Mungu na uhusiano wake na sayansi.

"Huu mfumo wa kupendeza kuliko yote wa jua, nyota sayari na vimondo, unaweza kutokea tu kutoka kwa maamuzi na utawala wa mtu Mtu mwenye akili na nguvu."
- Isaac Newton (Mwana mahesabu, Mnajimu, mwana fizikia, mwanasayansi mwenye ushawishi kuliko wote nyakati zote).

 "Kitabu cha asili ambacho lazima tukisome kimeandikwa na kidole cha Mungu"
- Michael Faraday (Mwanasayansi na mtaalam wa mambo ya usumaku na umeme-kemikali. Mmoja kati ya wanasayansi mahiri kabisa wa wakati wote)

"Fundisho la kuwa vitu kujiumba kwa vitu halitapona kutoka katika pigo la mauti lililoletwa na jaribio hili dogo"
- Louis Pateur (Mwana kemia na baiolojia ya viumbe wadogo. Mgunduzi wa kanuni za chanjo na mengine)

Kama una swali tutumie kwa anuani Yetu hii. Pia usiache kusome kipande kifupi cha Yesu Kristo