Monday, April 20, 2015

Mjue Roho Mtakatifu - 2 : Roho Mtakatifu ni Nani Kwetu Wanafunzi wa Yesu?

Katika sehemu ya kwanza tuliona watu wa imani mbalimbali wanamtambua Roho Mtakatifu kama nani. Katika dunia hii yenye imani nyingi, kila mtu akisema na lake, tunahitaji mamlaka ya mwisho ya kutuambia kipi ni sahihi na kipi si sahihi. Ashukuriwe Mungu ambaye hakutuacha bila ufunuo wa mamlaka ya mwisho: Neno lake, yaani Biblia Takatifu. 

Swali hili ni la muhimu sana kwa Wakristo kwa kuwa Yesu alipoondoka hakumkabidhi Kanisa awaye yeyote yule isipokuwa Roho. Kama tutakavyoona sehemu zijazo, hakuna Wokovu kwa mwanadamu pasipo Roho Mtakatifu wala hakuna maisha ya kushinda dhambi bila Roho Mtakatifu. Tatizo kubwa katika Kanisa la leo ni kuwa Roho Mtakatifu amefanywa kuwa “upako” na “nguvu” ambayo watu huitumia kwa faida yao wenyewe. Kwa mantiki hii haishangazi kuona “makanisa” mengi yamekosa nguvu na ushuhuda wa Yesu Kristo. Haya yote tutayaangalia kwa undani, lakini kwanza tujibu swali husika: Roho Mtakatifu ni nani kwa waamini? 

Utambulisho wa Yesu
Kabla ya kuondoka, Yesu alimtambulisha Roho kwa wanafunzi wake. Katika utambulisho huu aliourudia sehemu kadhaa, tunapata kujifunza juu ya umuhimu wa Roho wa Mungu. Huu ni moja ya mistari ambayo Yesu anamtambulisha Roho Mtakatifu kwetu:
Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. Mkinipenda, mtazishika amri zangu.Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. (Yohana 14:14-17)

Katika mambo yanayowatatiza wana wa Mungu ni jinsi watu wasio wanafunzi wa Yesu wanavyomdhihaki Roho Mtakatifu. Kwa Mkristo, Roho ni zaidi ya rafiki kwake, na hivyo ni haki yake kujisikia vibaya pale dhihaka na maneno mabaya yanaposemwa juu yake. Lakini Yesu alisema wazi kuwa ulimwengu sio tu hauwezi kumpokea bali haumwoni wala kumtambua. Kwa maana hiyo ni ujinga wa kutomtambua wala kumwona ndio chanzo. Shetani, mungu wa dunia hii, amewafumba macho yao hata wasione. Huyu ni Roho wa kweli. Na kwa sababu dunia yakaa chini ya mwovu (1 Yoh 5:19) aliye baba wa uongo (Yoh 8:44) lazima dunia na wana wake watamchukia.

Kwa hiyo ni kazi yetu kuendelea kuihubiri Injili ya Kristo itakayowafumbua macho ili nao wamwone na kumpokea Roho Mtakatifu.

Katika mstari huu pia Yesu anaweka wazi kuwa sisi, Wanafunzi wake, inatupasa kumtambua kwa maana akaa kwetu na Yu ndani yetu. Hatarajii kuondoka kesho au wiki ijayo. Yupo kukaa nasi milele. Neno linalotia hamasa ni pale Yesu anapomsema Roho kuwa ni msaidizi mwingine. Lugha yetu ya kiswahili ni changa ukilinganisha na Kiyunani, ambacho agano jipya limeandikwa kwalo. Neno msaidizi (parakletos) lina maana ya mtu aliyetumwa kumsaidia mwingine katika mwendo wake. Lakini pia lina maana ya msaidizi wa kisheria, yaani wakili.

Na tuangalie kazi hizi mbili muhimu za Roho Mtakatifu kwa mwamini, ambazo Yesu anatufundisha kuhusu Roho Mtakatifu katika mstari huu.

1. Msaidizi katika Mwendo/Safari
Kila mwanadamu aliyemwamini Yesu kama Mwokozi na Bosi wa maisha yake, ana safari. Sisi ni wapitaji duniani na hapa hatuna mji udumuo (2 Pet 2:11, Ebr 13:14). Katika safari hii kuna kuchoka, kukata tamaa na nyakati zingine hata mbele huoni. Ni katika safari hii, ambayo tunakabiliana na majaribu, na wakuu wa giza, tunahitaji msaidizi anayeijua njia na mbinu za kupanga vita. Ashukuriwe Baba wa Mbinguni ambaye hakutuacha yatima akatuachia Roho wa Kristo.

Huwa kuna nyakati napata shida pale ambapo wakristo tunawageuza viongozi wetu ndio Roho Mtakatifu. Ni vyema sana kuwategemea viongozi wetu kwa kadri ya mamlaka waliyopewa na Mungu mwenyewe (mf. Ebr 13:17). Lakini pale tunapowageuza wao kuwa ndio wasaidizi wanaochukua nafasi ya Roho, tunakuwa tunajipalia makaa wenyewe. Watumishi wa Mungu watabaki kuwa ni wanadamu, na msaada wao kwetu una kikomo.

Mathalani Roho anajua kazi yako iko wapi, au ni nani anakufaa kama mke/mume bora, na hata gari unayopaswa kupanda kwenda kazini. Lakini cha ajabu ni kuwa baada ya kunywa kila mafuta, kupakwa kila chumvi “ya upako” na kufanya kila “uaguzi uliorohoishwa” na vyote hivyo kushindwa, ndipo kumbukumbu kuwa Roho Mtakatifu yupo inarudi. Laiti ungeanzia kwa Roho Mtakatifu, kuna mambo usingeyapitia na maumivu mengi ungeyakwepa! Kwa nini unataabika na una msaidizi aliye na jibu pembeni yako?

2. Wakili wetu kwa Baba
Roho Yeye ni Parakleto, wakili wetu mbele za Baba. Biblia inatuambia wazi kuwa :
Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. (Rum 8:26)
Ukiwa mbele ya hakimu unahitaji wakili kwa kuwa huijui lugha ya kisheria na hivyo unahitaji msaidizi, atakayeweza kukusikiliza na kujua unachokihitaji na yeye kusimama mahakamani badala yako. Wakati mwingine hata mshitakiwa hajui anachohitaji na anachodhani anahitaji huwa sicho anachohitaji. Katika hali hii, wakili anahitaji kuchimba kwa undani sana na kujua kinachotakiwa kufanyika ili kumsaidia mtu husika.

Ndivyo afanyavyo Roho wa Kristo kwetu. Tunapokwenda kuomba, mara nyingi hatujui tunachopaswa kuomba. Wakati mwingine unapaswa kuomba hekima, lakini unachowaza ni kuomba gari au mume/mke. Roho anatusaidia kuomba tunachopaswa kuomba, na kwa kuwa anakaa ndani yetu anajua mahitaji Yetu ya ndani sana.

Ndio maana maisha ya Kikristo hayawezekani bila Roho wa Mungu kukaa ndani yako. Utabakia kujiita Mkristo lakini kila mtu atajua kuwa wewe siye mfuasi wa Kristo, maana kwa matunda mti hujulikana!

Baada ya utangulizi huu mfupi wa Roho Mtakatifu kutoka kwa Yesu mweyewe, ni wakati muafaka wa kuingia ndani zaidi ili kujua Utu na kazi zake. Jambo la kumalizia hapa ni kukukumbusha ndugu yangu msomaji kuwa Kama haujamjua Yesu bado kama Mwokozi wako binafsi, somo hili hutalielewa, na utaona kama hadithi tu.

Ukae ukijua siku yaja ambapo utaondoka dunia hii na kurudi kwake aliyekuumba. Naye atakuhukumu kwa namna ulivyoishi duniani. Matendo yako hayatamrubuni Muumba ili asikulipe kwa mabaya uliyotenda. Dawa pekee ya makosa yako ni kuikubali kazi ya msalaba wa Kristo, pale alipochukua dhambi za ulimwengu na kubeba adhabu yake. Ni hiyari yako au kuiamini kazi ya Kristo na kutubu mbele za Mungu, yaani kugeuka na kuamua kuacha njia zako mbaya ili uokoke na moto wa milele.

Maana “ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.” Ndipo atakapokujia Roho Mtakatifu na kukaa nawe milele kama arabuni ya ukombozi wa Mungu kwako!

Nitafurahi kusikia maswali yanayokutatiza na ningependa kuyajibu kwa kadri ya Neema aliyonijalia Roho wa Bwana. Mpaka sehemu ya Tatu ya somo hili,

Mungu akubariki