Saturday, May 2, 2015

Swali #2 Melkizedeki ni Nani?

Swali hili limekuwa likijirudia kwa karne nyingi sasa, na nadhani ni wakati sahihi, kama walivyofanya Wakristo wengine karne zilizopita, nikaweka mchango wangu wa uelewa wangu juu ya Biblia. Baada ya kujifunza toka kwao na kuyachunguza maandiko binafsi, nina hakika kuwa mchango wangu huu utawasaidia wenye kiu ya kujua Neno la Mungu zaidi. Usijekosea ukadhani ninajua kila kitu au ya kuwa nina "upako maalum", la hasha! Neno la Mungu linatufundisha kuwa Wanafunzi wa Neno, tusio na sababu ya kutahayari (2Tim 2:15). Kwa hiyo kama ulivyo ndivyo nilivyo na ndivyo tulivyo: wanafunzi wa Bwana Yesu.

Baada ya utangulizi huu, hebu na tuliangalie swali husika: Melkizedeki ni nani?

Kulingana na Program ninayotumia kujifunzia, neno Melkizedeki limeonekana katika Biblia mara kumi (Mwa 14:18, Zab 110:4, Kitabu cha Waebrania - 5:6, 5:10, 6:20, 7:1, 7:10, 7:11, 7:15, 7:17). Tatizo kubwa katika kumfahamu huyu mtu ni kuwa anaibuka kama mvuke na kuyeyuka kama barafu, hivyo kuna mengi ambayo inakuwa vigumu kuyafahamu kwa hakika. Ili kuchanganua vema nimeligawa jibu katika sehemu kuu tatu: tunachokijua, kilicho na utata na mtazamo wangu.
(a) Tunachokijua kuhusu Melkizedeki

Mwanzo 14:18, bila taarifa ya kabla inamleta katika picha Melkizedeki. Hebu tuone tunapata nini katika andiko hili:
Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani.   Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski.  Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu.  Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme.  Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana.  (Mwa 14:14 - 18)

Tunaona sifa mbili za Melkizedeki, kwanza mfalme na pili ni kuhani wa Mungu aliye juu. Salem ndiyo eneo ambalo mfalme huyu alitawala kulingana na mstari huu.  Salem ina maana ya amani. Kwa hiyo Melkizedeki alikuwa mtawala wa sehemu yenye jina lenye tafsiri ya amani. Akiwa kama kuhani, anambariki Ibrahimu na anapokea zaka za Ibrahimu  (mst 19-20).

Baada ya kitabu cha Mwanzo, jina la Melkizedeki tunalikuta Zaburi 110:4. Kabla hatujaiangalia Zaburi hii ni vyema machache yakasemwa juu yake. Mwandishi wa zaburi hii ni Daudi na anaiandika kama "Neno la Bwana kwa Bwana wangu". Bwana wa kwanza wa Daudi anamwambia Bwana wa pili, katika mistari saba ya zaburi hii. Na sehemu ya maneno ya Bwana kwenda kwa Bwana ni yale ya mstari wa nne ambayo ndiyo tutayaangalia kwa sasa:
Bwana ameapa, Wala hataghairi, Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki (Zaburi 110:4)

Kwa hiyo Bwana anaambiwa na Bwana kuwa yeye ni kuhani (sio atakuwa kuhani), mfano wa Melkizedeki. Neno mfano wa ni dibrâh  ambalo lina maana ya "utaratibu wa kufuata" au "namna ya". Kwa hiyo Bwana ni kuhani kwa mpangilio au utaratibu uleule wa Melkizedeki, mfalme wa Salem. Ingawa hakuna mengi sana tuyapatayo hapa kuhusu Melkizedeki, ila machache tunayapata.

Moja ni kuwa Melkizedeki sio mfano au roho, ila ni mtu halisi. Hii inatufanya tujue kuwa Mwanzo 14:18 inaongelea historia na si mfano kutoka hewani. Lakini pia ukuhani wake ni halisi na sio aina fulani ya mfano usio halisi (abstract title).

Hizi ndizo sehemu mbili pekee ambazo tunaziona katika Agano la kale. Sasa na tuangalie kitabu pekee cha agano jipya kinachotuambia habari za Melkizedeki. Sehemu ya kwanza jina Melkizedeki liaonekana katika agano jipya ni Ebr 5:6 amabapo ni nukuu ya Zab 110:4 ikitupa majibu ya Bwana anayeambiwa na Bwana kuwa ni Yesu Kristo. Hicho ndicho tunachokipata katika mstari huu. Mstari wa 10 sura hii hii unatupa picha ya Melkizedeki kuwa hakuwa kuhani wa kawaida, bali kuhani mkuu. Sura 6:20 inarudia kusisitiza kile sura ya 5:6 kinasema, kuwa, Yesu ni kuhani mkuu mfano wa Melkizedeki.

Sura ya saba inatupa historia ya Melkizedeki kwa kina kidogo kuliko Zaburi 110 na Waebrania 5 na 6. Haya ni mambo tunayoyapata sura ya 7:1-17:
  • Melkizedeki ni halisi kama alivyokuwa Ibrahimu 
  • Maana ya Jina Melkizedeki ni mfalme wa haki na Salem maana yake ni amani
  • Alikuwa kuhani aliyepokea zaka, ukuhani wake ni tofauti na ule wa Walawi

Kwa hiyo tunajua bila shaka kuwa Melkizedeki alikuwa ni mtu halisi na sio kisasili, na alikuwa kuhani mkuu. Melkizedeki ni jina lenye maana ya Mfalme wa haki, tena Mfalme wa salem ina maana ya Mfalme wa amani.

Baada ya kuyaona yale yaliyo bayana na tuhamie sehemu ngumu yenye mawazo mgawanyiko juu ya utambulisho na asili ya Melkizedeki.
(a) Utata wa Utambulisho wa Melkizedeki na Mtazamo wangu

Kwa sababu Katika kitabu cha Mwanzo hatuna maelezo ya kutosha kumhusu huyu mtu, tutategemea sana Waraka wa Waebrania kujua juu ya utambulisho wake. Kumbuka kuwa mwandishi wa kitabu hiki ni Myahudi mzuri ambaye alikuwa na nafasi ya kusoma maandiko ya kihistoria ya Wayahudi ambayo leo hatuna baada ya hekalu kuchomwa moto. Hivyo basi lazima katika kusoma kwetu tusijifanye kujua kuliko mwandishi bali tujaribu kwa kadri ya uwezo wetu kuelewa alichomaanisha mwandishi.

(i) Nini Mwanzo wa Melkizedeki?
Kuna mawazo ya aina mbili hapa. La kwanza ni kuwa Melkizedeki alikuwa mwanadamu na mfalme wa Salem. Wengine (nikiwemo mimi) huamini kuwa maelezo ya Biblia kuhusu Melkizedeki yanabeba vitu ambavyo mwanadamu hawezi kuwa navyo. Mathalani Ebr 7:3 inatuambia kuwa yeye hana baba wala mama naye ni kuhani milele. Wandugu wanaotafsiri kuwa ni mwanadamu hudai kuwa andiko hili lina maana ya kuwa kumbukumbu zake kuhusu uzao na wazazi wake hazipo na kwamba umilele wa ukuhani wake ni kuweka mkazo na si vinginevyo.

Binafsi naona msimamo huu una mapungufu mengi sana. Kwanza Biblia iko wazi kuwa hana wazazi (na sio hana kumbukumbu ya wazazi) na kuonesha hilo imeweka wazi kuwa hana baba wala mama. Lakini kuonesha sio mwanadamu maandiko yameweka wazi kuwa " hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake"  Kwa maana nyingine ni kuwa amekuwapo siku zote na uhai wake upo ndani yake Mwenyewe.

(ii) Melkizedeki ni Nani?
Baada ya kuona maandiko yanasema nini juu ya Melkizedeki ni wakati wa kuvumbua utambulisho wake. Kwa kuwa Mtu huyu hana mwazo wa siku wala mwisho wake (wa milele), kama ulivyo ukuhani wake, basi yeye ni Mungu. Ni Mungu peke yake ndio hana mwanzo wala mwisho. Pia ni Mungu pekee uhai wake uko ndani yake, na hivyo kwa kuwa hana mwanzo wala mwisho vivyo hivyo na uhai wake!

Yohana 1 inatuelezea habari za Neno nayo inasema "Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima" (mst 4) na Yoh 1:1 inaweka wazi kuwa kabla ya Mwanzo neno alikuwepo. Kwa hiyo kwa kwa uelewa wangu wa Biblia Takatifu ni kuwa Melkizedeki ni Mwana wa Mungu kabla hajauvaa mwili na kuitwa Yesu. Hii sio mara ya kwanza kwa Kristo, Masihi (Bwana wa pili katika Zab 110), kuwatokea  wanadamu katika mwili. Alimtokea Ibrahimu akiwa na malaika wawili (Mwanzo 18)

(iii) Vipi wanaoamini Melkizedeki ni mwanadamu?
Kama ni swali la kuhusu tafsiri yao, ninaamini wanakosea kutafsiri maandiko. Lakini kama ni swali la kama wanakwenda mbinguni au motoni jibu ni kuwa haihusiani na safari hii. Kuna watu hawajui hata habari za Melkizedeki a tutakutana nao mbinguni na wengine wanajua kwa usahihi lakini, kwa huzuni, watakwenda Jehanamu. Hii ni kwa sababu njia ya kwenda mbinguni si kujua juu ya Melkizedeki au mtu mwingine yeyote bali ni kutubu dhambi zako mbele za Mungu na kumwamini Yesu Kristo na kazi aliyofanya pale msalabani kulipa deni ya dhambi yako. Hii ndio tofauti ya waendao mbinguni na Jehanamu: Yesu Kristo!

Kwa hiyo, kama una elimu sahihi juu ya tafsiri ya biblia, jua haitakusaidia kama dhambi zako hazijasamehewa bado. Utubu sasa na kumwamini Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Nani ajua kuwa maneno haya yanaweza kuwa ya mwisho kuyasoma kabla hujapita mlango wa mauti kukutana na Mungu wako?
"Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka." (Warumi 10:9)

No comments:

Post a Comment