Baada ya haya
nikasikia sauti kama sauti ya umati mkubwa wa watu mbinguni
ikisema kwa nguvu : “Haleluya! Wokovu na utukufu na uweza
ni vya Mungu wetu, kwa maana hukumu Zake ni za kweli na za haki.
Amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeuharibu ulimwengu kwa uzinzi wake.
Mungu amemlipiza kisasi kwa ajili ya damu ya watumishi wake.’’
Wakasema tena kwa
nguvu: “Haleluya! Moshi wake huyo kahaba unapanda juu
milele na milele.’’
Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wenye
uhai wanne wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu,
aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti
kuu: ‘‘Amen! Haleluya!’’
Kisha sauti ikatoka
katika kile kiti cha enzi, ikisema: ‘‘Msifuni Mungu wetu,
ninyi watumishi wake wote, ninyi nyote mnaomcha, wadogo kwa
wakubwa!’’
Kisha nikasikia
sauti kama sauti ya umati mkubwa wa watu, kama sauti ya maji
mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi ikisema:
‘‘Haleluya! Kwa maana Bwana Mungu wetu Mwenyezi anamiliki.
Tufurahi, tushangilie na kumpa utukufu!
Kwa maana arusi ya
Mwana-Kondoo Imewadia, na bibi arusi wake amejiweka tayari.
Akapewa kitani safi,
nyeupe inayong'aa ili avae.’’ (Hiyo kitani safi inawakilisha
matendo ya haki ya
watakatifu.)
- Ufunuo 19: 1 –
8
1. MAANA YA NENO
HALELUYA
Kwa baadhi ya watu
Neno Haleluya ni moja ya maarufu sana katika kujaribia kipaza sauti.
Ikikolezwa na “Bwana Yesu Asifiwe” basi inafaa sana kwa kujaribia
kama mitambo ya sauti imekaa sawa. Kwa wengine ni sehemu ya
kuwalazimisha “walokole wenye masikio ya utafiti” wawasaidie
katika kupata umaarufu wao. Na kwa wengine ni neno ambalo kama maneno
ya kuimba yamewaishia basi ndio neno sahihi la kurefusha wimbo ili
kumalizia dakika walizopewa kuimba.
Kuna ufahamu anuai
juu ya neno Haleluya ambao wakati mwingine umeleta makwazo na
maumivu, huku wakati mwingine ukiwapa wengine “hatua” ambazo
wako tayari kuzipata kwa gharama yeyote. Vyovyote iwavyo neno
Haleluya lina asili na maana yake halisi. Swali la msingi hapa si
kama Haleluya inasemwa na kuimbwa namna gani bali ni nini maana
ya neno hili na nani haswa anapaswa kulisema ama kuliimba!
Katika agano la
Kale, ambalo kwa sehemu kubwa limeandikwa Kiebrania, neno Haleluya ni
mkusanyiko wa maneno mawili “Hallelu” lenye maana “(Ninyi)
msifuni” na “Yah” lenye kubeba Jina la Mungu wa Israeli, yaani
Yahwe. Kwa hiyo katika matumizi yake katika agano hilo (na Biblia kwa
ujumla) ina maana Msifuni (ninyi) Yahwe ikiwa ni neno ambalo linatoa
amri (imperative). Katika Agano Jipya ambalo limeandikwa kwa
Kiyunani, Neno hili “Alleluia” lina maana sawa na ile ya
Kiebrania.
2. UZITO WA NENO HALELUYA
Wengi wamelitumia
neno Haleluya vibaya. Hii ni kwa sababu ya Ujinga wa maana na uzito
halisi wa neno hili. Haleluya ni Neno alilolichagua Mungu aliyeumba
mbingu na dunia kama neno la amri kwa ajili ya sifa na utukufu wake.
Huyu si mungu kama ilivyo miungu ya dunia hii isiyo na idadi, bali ni
Mungu ambaye Uweza wote na Utukufu ni wake peke yake. Ni Mungu
ambaye Hukumu zake ni za haki.
Ni Mungu aliyeona
maovu ya dunia nyakati za Nuhu na akaangamiza “Kila kitu chenye
uhai juu ya uso wa nchi kilifutiliwa mbali, watu, wanyama, viumbe
vitambaavyo na ndege warukao angani wakafutiliwa mbali toka duniani”
(Mwanzo 7:23). Ni yule ambaye aliangamiza miji ya Sodoma na Gomora na
hata leo tuna ushahidi wake. Si Mungu ambaye unaweza mchezea wala
kumtetea. Yeye ndiye Mungu mkuu, Muumba na Mmiliki wa vyote ikiwemo
nyumba yako, ukoo wako, mali zako na uhai wako.
Hukumu za Mungu wetu
ni za Haki na hapepesi macho wala kufumbia macho uovu wowote. Kama
alivyoihukumu dunia ya enzi za Nuhu ndivyo atakavyomhukumu kila mmoja
wetu kwa kuvunja sheria yake. Kwa wizi uwe “mdogo” wa kalamu au
“mkubwa” wa ujambazi, tamaa ya macho, ulevi, uzinzi na kila
ambalo Yeye kama mmiliki halali wa wanadamu wote ametukataza
tusifanye. Yeye ni Yah katika Haleluya ambaye hatupaswi kulitaja jina
lake bure kama sehemu ya kutafutia umaarufu, kujaribia vipaza au
namna yeyote ya kulishusha jina lake. Jina lake ni kuu sana na lafaa
kuheshimiwa na kila kitu na kila mtu.
Kwa hiyo Neno
Haleluya linapaswa kutamkwa tu pale ambapo tunamsifu Mungu aliye hai
na si vinginevyo. Kumbuka Neno hili limebeba Jina Takatifu sana la
Mungu ambaye alisema wazi bila kificho “Usilitaje jina la BWANA
Mungu wako bure, kwa kuwa BWANA hataacha kumhesabia hatia yeye
alitajaye jina lake bure” (Kumb 5:11). Kwa hiyo ni kosa kubwa
kulitumia Jina la Mungu Muumba wa Mbingu na nchi, ambaye uhai wako
uko mikononi mwake, naye utakutana nae nukta moja baada ya kifo
chako. Ni hatari sana, na ni upumbavu mkuu kujitia katika hatari hii.
3. HAKI YA
KULITUMIA NENO HALELUYA
Kutokana na asili na
maana ya neno Haleluya, sio kila mtu ana haki ya kulitamka. Biblia
imeweka wazi kuwa ‘‘Msifuni Mungu wetu, ninyi watumishi wake
wote, ninyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa!’’ (Ufu 19:5).
Ni watumishi wa Mungu pekee, wakubwa kwa wadogo wanaopaswa na
kuruhusiwa kulitamka hili neno bila hofu ya kujiletea hatia juu ya
vichwa vyao. Hii ni kwa sababu watumishi wa Mungu aliye hai ni sehemu
ya Kanisa, yaani Bibi-Harusi wa Kristo ambaye ameandaliwa karamu kuu
mbinguni ilhali wengine wote sehemu yao ni katika ziwa la moto.
“Kisha
nikaona kiti kikubwa cha enzi cheupe, dunia na mbingu
zikaukimbia uso wake Yeye aliyeketi juu yake, wala mahali
pao hapakuonekana. Nami nikawaona wafu wakubwa na
wadogo, wakiwa wamesimama mbele ya hicho kiti cha
enzi na vitabu vikafunguliwa. Pia kitabu kingine
kikafunguliwa ambacho ni cha uzima. Hao wafu wakahukumiwa sawasawa
na matendo yao kama yaliyoandikwa ndani ya hivyo
vitabu... Iwapo mtu jina lake halikuonekana katika kile
kitabu cha uzima, alitupwa ndani ya lile ziwa la moto. (Ufu
20:11-15)
Kama wewe si sehemu
ya Watumishi wa Mungu, basi ujue sehemu yako ni Jehanamu iwakayo
moto. Je, utapata faida gani kufurahia maisha ya dhambi miaka hata
mia, kama Mungu atakupa kuifikia na kisha baada ya hapo kupotelea
kwenye maumivu milele? Kwa nini upotelee “Mahali ambako ‘funza
wake hawafi, wala moto hauzimiki’”?
Jehanamu ipo, na
wanaokwenda huko wapo (na wengine walishafika). Je huoni kama ni
wakati wa kutafakari kama kweli umekubali kwa moyo wako wote kuishia
motoni milele?
Pengine unajisemea kuwa huu ni upuuzi! Kama ndivyo, Neno la Mungu
lina habari njema nawe. Linakwambia hivi: “Atendaye mabaya na
aendelee kutenda mabaya, aliye mchafu na aendelee kuwa
mchafu...” (Ufu 22:11). Kwa maana nyingine ni kuwa
endelea kuponda maisha Jehanamu ya moto inakusubiria, na wakati wako
utafika wala hakutakuwa na wa kukuokoa!
Kwako wewe ambaye
unaona huwezi kukubali kwenda Jehanamu nina habari mbaya na kisha
njema. Habari mbaya ni kuwa tayari uko njiani kwenda Jehanamu na
Mungu akiamua wakati wowote kuondoa pumzi yake ya uhai aliyokupa,
utaamkia kuzimu kusubiria hukumu yako ya mwisho, yaani Jehanamu ya
Moto. Hauna jinsi ya kujisaidia na deni la kuvunja amri ya Mungu
hauwezi kulilipa milele yote.
Habari njema ni kuwa
hauna ulazima wa kulilipa wewe. Mungu katika huruma na rehema zake,
aliamua kuibeba hukumu ya hatia yako yote. Katika kulitimiza hilo
aliamua kuongeza uanadamu katika Uungu wake na akakaa nasi katika Utu
wa Yesu Kristo. Akaishi miaka 33 bila kutenda dhambi yoyote na hivyo
hakustahili kufa, maana mshahara wa dhambi ni mauti. Lakini kwa
kukupenda wewe akaamua kufa akibeba adhabu uliyoistahili ili wewe uwe
na Uzima alioustahili, tena uzima wa milele.
Kwa kuwa Alikuwa (na
hata leo ni) Mungu, aliweza kubeba adhabu ya dunia nzima kwa kipindi
kile. Kisha akazikwa na siku ya tatu akafufuka akitangaza ushindi juu
ya kifo na mauti.
Deni hilo halilipwi
tu kiautomatiki. Malipo yanamhusu kila anayekiri kuwa Yesu ni Bwana
Mungu wake na kuwa Mungu Baba alimfufua toka kwa Wafu, na kisha
kuamua kuacha njia za dhambi na kumlilia Yesu amuokoe. Basi kwake
huyo deni lake litasamehewa na Jina lake litaandikwa katika kitabu
cha Uzima.
Huna muda wa
kupoteza kama unazitaka rehema za Mungu kabla hujachelewa. Hapo ulipo
omba toba na rehema toka kwa Mungu wako aliyekuumba, Yesu Kristo.
Hakuna namna nyingine ya kuepuka Jehanamu ya moto isipokuwa hii tu.
Ni njia pekee ya kukufanya uwe sehemu ya Kanisa, yaani Bibi harusi wa
Kristo, na kuwa na uhakika wa kuwepo katika sherehe kubwa sana ijayo
huko Mbinguni. Huko tutaimba Haleluya kwa Mungu wetu, na kwa
Mwanakondoo wa Mungu aliyekufa kwa mateso ili atuokoe na Jehanamu!
Naam! Utakuwa sehemu
ya kile Mtume Yohana alichokisikia kuwa kuwa ni “sauti kama sauti
ya umati mkubwa wa watu, kama sauti ya maji mengi yaendayo
kasi na kama ngurumo kubwa ya radi ikisema: ‘‘Haleluya!
Kwa maana Bwana Mungu wetu Mwenyezi anamiliki. Tufurahi,
tushangilie na kumpa utukufu!
Na haitakuhitaji
usubiri kufika Mbinguni ndipo uimbe haleluya, kwa sababu Bwana
atakusamehe dhambi zako zote, nawe utaimba “Haleluya, wewe ni Mungu
Mwokozi”. Na tena Bwana atakuongoza na kukufundisha njia ya
kuiendea nawe Utasema, “Haleluya, Bwana unastahili!”. Na Yote
katika Yote utagundua kuwa na utatamani kuwaambia wengine
Hallelu-Yah, yaani msifuni ninyi Bwana Mungu wetu
....
Haleluya, Amen!