Sunday, April 2, 2017

Swali #4 - Maji ya kipindi cha Nuhu kutengeneza Safina yalienda wapi?

Nimekutana na hili swali likiwa limeulizwa na mwanachama wa JamiiForums. Swali lenyewe linasema hivi:

Kwa muda sasa najaribu kujiuliza hili swala kwamba Bahari ilikuwepo tangu kuumbwa kwa hii dunia ila maji yalioangamiza kizazi cha enzi za Nuhu yalipotelea wapi katika uso wa dunia au ndio kusema kina cha bahari kiliongezeka? Mwenye uelewa juu ya hili naomba anisaidie.

Nimesoma majibu mengi nikaona kuna uhitaji wa kuja na jibu ambalo ni sahihi badala ya kejeli na mashambulizi kwa muuliza swali. Swali hili sio jipya na limeulizwa kizazi hadi kizazi, na kama ilivyo ada, Biblia imeendelea kuonesha kuwa ni Neno la Mungu kwa kutoa majibu ambayo ni sahihi na yasiyobadilika licha ya uelewa wetu kubadilika.

Gharika ya nyakati za Nuhu yalikuwa ni dunia nzima kama Biblia isemavyo wazi kabisa:

" Ile gharika ilikuwako juu ya nchi siku arobaini; nayo maji yakazidi, yakaieleza safina, ikaelea juu ya nchi. Maji yakapata nguvu, yakazidi sana juu ya nchi; na ile safina ikaelea juu ya uso wa maji. Maji yakapata nguvu sana sana juu ya nchi; na milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu ikafunikizwa. Maji yakapata nguvu, hata ikafunikwa milima kiasi cha mikono kumi na mitano."
- Mwanzo 7:17 - 20

Kwa maneno rahisi ni kuwa ukiondoa Safina, hakuna kilichokuwa juu ya maji. Vyote vilifunikwa ikiwemo milima, miti, n.k. Sasa kila mwenye kufikiri atajiuliza, hayo maji yaliyofunika mpaka milima yalikwenda wapi? Maana kama ni bahari Biblia inasema zilikuwepo kabla ya gharika (Mwanzo 1: 9, 10). Kwa hiyo lazima kuna jibu kuhusu hili.

Dhahania Nyuma ya Swali
Kwa sababu swali limeulizwa katika sehemu ambayo ni ya maswali na majibu ni vyema nikachokonoa dhahania ambazo inawezekana muuliza swali na zingine toka kwa baadhi ya waliochangia ili kuweka rekodi sawa. Kwanza kuna dhahania kuwa Biblia ni hadithi na visasili ambavyo havifai kusikilizwa na watu makini. Hii ni dhahania ambayo nimekutana nayo karibu katika kila swali linalojadiliwa kuhusisha Biblia.

Kama ambavyo nimegusa katika baadhi ya maandiko yangu katika wavuti hii na katika ukurasa wetu wa Facebook, Biblia si tu iko sahihi juu ya mambo yote inayoelezea bali ni Neno la Mungu kwa wanadamu, na lenye ujumbe maalum ambao anapenda wote wausikie. Hilo tutaliangalia baadaye. Itoshe tu kusema wanaosema Biblia ni mkusanyiko wa visasili au kwamba haiwezi kuaminika, ni wale ambao aidha wana chuki au hawajafanya utafiti na kuichunguza na kuijua.

Dhahania ya pili ni kuwa sura ya nchi kabla ya gharika ilikuwa sawa na sura ya nchi ya leo. Kwamba mabonde kama Ngorongoro yalikuwapo kama ambavyo milima mirefu kama Kilimanjaro ilikuwepo. Hii ni dhahania isyo na ushahidi wowote. Kiukweli hatujui malima mrefu kuliko yote kabla ya gharika ulikuwa na urefu kiasi gani. Lakini kulingana na Biblia, japo hatujui haya yote, hii dhahania ni potofu kwa maana gharika ilibadili kabisa sura ya nchi dunia yote. Biblia inasema:

"Ikawa baada ya siku hizo saba, maji ya gharika yakawa juu ya nchi. Katika mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, mwezi wa pili, siku ya kumi na saba ya mwezi, siku ile chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu, madirisha ya mbinguni yakafunguka."
- Mwanzo 7:10 -11

Mistari hii hii inaonesha kuwa kulikuwa na mpasuko wa ardhi uliosababisha maji chini ya ardhi kububujika kwa nguvu. Kwa sababu hili sio andiko juu ya gharika ilivyotokea, itoshe tu kusema kuwa kupasukapasuka kwa ardhi na mabubujiko ya nguvu yalibadilisha sura ya nchi.

Kwa Hiyo Maji yalienda Wapi?
Jibu lipo katika mistari mingi ya Biblia leo nitagusia mmoja.

" Uliiweka nchi juu ya misingi yake, Isitikisike milele. Uliifunika kwa vilindi kama kwa vazi, Maji yalikuwa yakisimama juu ya milima. Kwa kukemea kwako yakakimbia, Kwa sauti ya radi yako yakaenda zake kasi, Yakapanda milima, yakatelemka mabondeni, Mpaka mahali ulipoyatengenezea. Umeweka mpaka yasiupite, Wala yasirudi kuifunikiza nchi."
 - Zaburi 104:5-9

Katika andiko hili tunaona dunia kwa ufupi. Kwamba Mungu aliiumba na baadaye kuifunika kwa vilindi kama tulivyosoma hapo juu, ambapo maji yalikuwa yakisimama juu ya milima. Sehemu ya pili inatuambia kwa "kukemea" kwake Bwana na kwa "sauti ya radi" zake yakaenda kwa kasi mpaka mahali alipoyatengenezea, na akaweka mpaka yasirudi kuifunikiza nchi.

Kwa mtu anayefahamu kuhusu elimu ya miamba (geology) atakuwa ameelewa jibu hili. Nitajaribu kulirahisisha kwa ajili ya wasomaji wangu. Lakini kujibu swali husika ni kuwa "Maji yale yapo, ila yalihamishwa na kuwekwa mahali, hapa hapa duniani".

Gharika kubwa kama ya nyakati za Nuhu lazima isababishe mvurugano na mtitiriko wa nguvu wa maji mengi. Athari za maji kutiririka kwa namna hii huwa ni kusawazisha sehemu nyingi zilizoinuka hasa kwa maji yaliyodumu siku mia hamsini. Kwa hiyo lazima kukemea huku na radi hizi inamaanisha tukio la nguvu ambalo lilisababisha maji kuanza kutembea kwa kasi mpaka yalipofika mahali yalipowekwa hata leo.

Wanasayansi wa Kikristo wamefanya tafiti mbalimbali kujua kama wanaweza kujua angalau namna na mahali yalipo maji hayo. majibu ya tafiti hizi ni kuwa Bwana Mungu alifanya jambo ambalo lilisababisha kubonyea kwa gamba la dunia (earth's crust) na kusababisha sakafu ya bahari kushuka chini na upande mwingine wa ardhi kupanda juu. Hivyo maji yakashuka huko na mpaka leo yapo huko baharini.

Matokeo haya yanakubaliana na ushahidi tulio nao. Kwa mfano juu ya mlima mrefu kuliko yote, Everest katika safu za milima himalaya, yamekutwa matamahuluku. Kwa hali ya hewa ya milima kama hii hatutarajii kuyakuta. jibu rahisi ni kuwa milima ukiwamo Everest ni matokeo ya matendo ya Mungu yaliyosababisha kuinuka kwa ardhi kuelekea mwishoni au baada ya gharika.

Lakini pia dunia ikiwekwa ulazo, maji yaliyopo yanatosha kuifunika yote kwa kilomita 1.7 - 3 kwa makadirio ya watafiti. Kwa hiyo Mungu aliibadili sura ya nchi na hivyo kuyahamisha maji yale.

Kwa kumalizia nikuulize swali. Ulishawahi kujiuliza kwa nini Mungu aliiangamiza dunia kwa gharika? Hilo ni swali la msingi sana na ningependa nikujibu. Ni kwa sababu uovu ulikuwa mwingi sana. Je waonaje leo? Uovu ni mwingi pia. Basi siku inakuja ambapo Mungu atawahukumu walio wafu na walio hai. Kila dhambi iwe ni uongo, wizi (hata wa pipi), uasherati, tamaa, chuki na nyinginezo zote zitahukumiwa.  Kama uliwahi kutenda dhambi hata moja tu maishani mwako, uko hatarini. Atakapohukumu utakuwa upande wa maumivu.

Lakini Yesu alikufa na kubeba dhambi ya ulimwengu wote, na ni Yeye pekee anaweza kukusamehe dhambi zako na kusimama kama wakili na mtetezi siku ile ya kutisha. Mwamini leo, tubu dhambi zako mbele zake. Geuka na kuacha njia mbaya na umtumainie Yesu pekee kwa wokovu wako hata siku ile. Kumbuka Biblia inasema:

" Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao..... Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto." - Ufunuo 20:11-15