Kwa wengine pasaka ni wakati wa
mapumziko ya kifamilia na kutafakari maendeleo yao, walipojikwaa na
wanapoelekea. Kwa wengine ni Wakati wa "kuponda mali, kufa
kwaja" na wapo ambao pasaka ni wakati wa kufikiria kuhusu dini
zao na kuangalia namna wanayoweza kujitengenezea mazingira ya kuzikwa
na dini zao wakifa. Lakini kwa wengine pia ni wakati wa kusherekea
ushindi wa Bwana na Mwokozi wao, Yesu Kristo.
Makundi yote haya, isipokuwa la mwisho,
hawako sahihi. Pasaka ni wakati mzuri wa kusherekea ushindi wa
Mwokozi wetu Yesu Kristo. Hili ni jambo la muhimu sana ambalo bila
hilo hakuna Pasaka. Swali la msingi ambalo nilikuwa nalitafakari hata
kunisukuma kuandika makala hii fupi sana ni hili "nini hasa moyo
wa Pasaka"? Ni kweli ni siku ya kufurahia ushindi, na ni kweli
kuwa Ukombozi wa Mwanadamu hautenganishwi na tukio hili. Lakini ni
nini moyo wa Pasaka hasa? Majibu ya tafakari hii ndiyo ninataka
nikushirikishe.
Mfululizo wa Matukio
Kabla sijaweka kile nimejifunza leo
hebu tuangalie kifupi matukio kuelekea pasaka. Yesu na wanafunzi wake
wako katika chakula cha jioni, huku shetani akiwa amekwisha uteka
moyo wa Yuda. Yesu hali akijua anahesabu masaa kabla ya kipigo,
maumivu na mateso, anawafundisha wanafunzi wake kutumikiana, akifanya
kazi iliyofanywa na watumwa, kuosha miguu ya wanafunzi wake. Petro
anajaribu kuzuia hili (Yoh 13:6-9) Bwana anamkemea na kuendelea na
kazi yake hiyo. Mwisho Yesu anawaambia wanafunzi kuwa Yuda Iskariote
atamsaliti na Yuda, kwa kuingiwa na shetani, anakwenda zake kulifanya
alilo kusudia moyoni mwake. Haya yote ni mfululizo wa matukio
kuelekea Pasaka, sura ya 13. Baada ya haya yote, inafuata sura
ambayo ina moyo hasa wa Pasaka!
Moyo wa Pasaka na kusudi la Mungu
Moyo wa pasaka umeambatana na kusudi la
Mungu la milele. Kabla hajaumba chochote, Mungu alijua mambo yote
ambayo yatatokea katika historia ya mwanadamu. Kwa sababu ya ufahamu
wake wa milele, usio na mwisho, Mungu aliumba akiwa na kusudi. Kusudi
hili ndio moyo wa Pasaka. Kifo cha Yesu Kristo, na kufufuka kwake,
vyote hivi ni njia za kufikia kusudi hili: Mahusiano ya Mungu na
mwanadamu. Hebu tusome maneno ya Yesu mwenyewe katika sura hii ya 14
ya Yohana:
"Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo" (Yoh 14:1 - 3)
Yesu anawaambia wanafunzi wake kuwa
wasifadhaike, na sababu ni kuwa anakwenda kuwaandalia mahali katika
makao ya mbinguni. Mstari huu unatupa moyo wa pasaka ni Mungu akae na
wanadamu. "Maana naenda kuwaandalia mahali", ni ahadi nzito
kabisa kuwa ipo siku inakuja ambapo wote tulio wanafunzi wa Yesu
Kristo tutakaribishwa naye kwa Baba yake. Ndiyo, Yesu Mwenyewe
anasema "nitakuja tena niwakaribishe kwangu". Huu ndiyo
moyo wa Pasaka.
Mungu alipomuumba mwanadamu, alikuwa
na ushirika naye wa namna ya ajabu kabisa. Hata pale Adamu na mkewe
walipoasi sheria ya Mungu bado Mungu aliwatembelea. "Kisha
wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua
kupunga" (Mwa 3:8). Mungu alimuumba Mwanadamu ili awe na
ushirika nae, na ndio maana akamuumba kwa mfano Wake na sura Yake
(Mwa 1:26-27). Kwa sababu ya kusudi hili Mungu alitembea na Henoko
miaka 300 (Mwa 5:22), Nuhu, Ibrahimu, Daudi na wengine wengi.
Ibrahimu, Biblia inatuambia, " alikuwa akiutazamia mji wenye
misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu" (Ebr
11:10). Ni Mji huu ambapo Mungu atakamilisha kusudi lake la milele,
ambapo "maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu" (ufu 21:3).
Yesu anaongelea makazi haya ambayo kwa
milenia mbili amekuwa akituandalia, ili alipo nasi tuwepo. Huu ndio
moyo wa Pasaka. Mungu aliamua kumtoa mwanawe wa pekee ili afe, ili
kwa kifo chake Yeye asiye na hatia, abebe hatia zetu zote na tuweze
kuwa na uhalali kwa kifo na damu yake, kuingia katika mji huu. Mauti
ya msalaba na ufufuko wa Yesu ulikuwa ni kutimiza kusudi hili na ndio
moyo halisi wa pasaka!
Katika sehemu ya pili tutamlizia kuona kwa nini na jambo hili lina maana gani kwako.
Amani ya Kristo, na Neema yake kuu iwe nawe, amen!
Stefano
Amani ya Kristo, na Neema yake kuu iwe nawe, amen!
Stefano
Soma Sehemu ya Pili hapa
No comments:
Post a Comment