Friday, April 18, 2014

Moyo wa Pasaka - Sehemu ya Mwisho

Katika sehemu ya kwanza tuliona kifupi ni nini moyo wa Pasaka kibiblia. Sehemu hii ya mwisho tutamalizia kuona kwa ndani zaidi maana ya pasaka kwako wewe binafsi. Karibu tuendelee...

Pasaka Ina Maana Gani Kwako?
Moyo huu wa pasaka una sura mbili. Sura ya kwanza ni ya tabasamu la bibi harusi akimsubiri Bwana harusi arudi mara amalizapo kujenga nyumba watakayokaa huko kwa Baba wa Bwana harusi. Bibi harusi anasubiri kwa hamu akichungulia chungulia aone kama Bwana wake yuaja. Akijiandaa na kuhakikisha yu msafi ili sekunde ile Bwana harusi atakayokuja amkute tayari. Sisi kama kanisa la Kristo, ambao tumemkiri na kumwamini Yesu awe si tu Mwokozi kwetu bali mtawala wa maisha yetu na bosi mkuu, tunaitwa ni bibi harusi, ambapo tunapaswa kuishi kwa utakatifu kama "bikira safi" (II Kor 11:2). Na ndipo tunasubiri siku ile ambapo tutasahau taabu na maumivu, na magonjwa na yote ya dunia hii, siku ile kuu ya kukutana na Bwana harusi, maana:

"Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele" (1Th 4:16 - 17)
 
Picha ya pili ni ya huzuni, mashaka na kukosa amani. Amini usiamini, pamoja na Mungu kuingia gharama ya kulipa deni la dhambi kuna watu wako wanaugulia maumivu Kuzimu, na wapo kati yetu, pengine hata ikawa ni wewe unayesoma, ambao wataingia Jehanamu ya moto. Kiburi cha kutotaka kushuka mbele za Muumba wako na kupenda kwako dhambi vitakuangamiza. Kwako mtu wa namna hii pasaka ni ujumbe wa machozi na majonzi.

Ina maana kuwa Yesu atakapokuja kuchukua bibi arusi wake, hautakuwa mmojawapo. Ni kweli unajidanganya kuwa wewe ni Mkristo huku ukijua toka katika moyo wako kuwa Yesu hakujui. Ndio, endelea kujifariji ila siku yaja ambapo Yesu anasema "Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu" (Matt 7:23). Usisherekee Pasaka maana moyo wa pasaka kwa watu wa aina yako ni tangazo la ole!

Si kwamba tu utakosa nafasi ya bibi arusi, lakini pia utapitia wakati mgumu sana duniani ikitokea ukawa hai. Mungu atauhukumu ulimwengu kwa dhiki kubwa sana ambayo haijawahi kuwepo wala baada ya hapo haitakuwapo. Itakuwa ni zaidi ya vita zote mbili za dunia. Na mwisho Yesu huyu ambaye tunasherekea pasaka leo ataweka kiti cha Enzi cha hukumu ili akuhukumu kwenda ziwa la moto, naam "Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto" (Ufu 20:15). Mpaka sasa sijaelewa unasherekea nini katika hali kama hii!

Ndio, sitaki nikufariji kwa maneno mfu maana Biblia iko wazi kuwa "Kwa maana [Mungu] ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu" (Mdo 17:31), ufufuo wa Yesu ambao unapanga kuusherekea ni uthibitisho kuwa utahukumiwa na Mungu kwenda ziwa la moto hakika, ni kipi cha kusherekea kwako?

Ushauri Mwema
Kwako wewe uliye kati ya bibi arusi, jiweke safi. Tengeneza mavazi yako ili akija sasa, uwe tayari kwenda nae kwa Baba yake. Kumbuka atakuja kuchukua kanisa safi, lisilo na makunyazi wala mawaa. Yesu Kristo anakuja!

Kwako wewe usiyeokoka, fanya hima ufanye amani na Muumba wako. Maana "ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka" (Rum 10:9). Unasema utafikiria? Hujui kama muda huu unaposoma hapa unaweza kuwa umebakiza dakika au hata sekunde chache kumaliza maisha yako? kumbuka baada ya kifo ni hukumu (Ebr 9:27). Fanya Uamuzi wa busara sasa. Chagua kuokoka na hasira ya Mungu ili pasaka iwe ni tabasamu kwako. Kwamba tutakaa na Mungu milele, ndio kusudi la Mungu na moyo wa pasaka!

Mungu akutunze na kukubariki!
Stefano


No comments:

Post a Comment