Swali
Danieli Sura ya Tano inasema Belshaza
ndiye alikuwa mfalme wa mwisho wa Wakaldayo. “Usiku huo huo
Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa. Na Dario, Mmedi, akaupokea
ufalme, naye umri wake alikuwa na miaka sitini na miwili.” (Dan
5:30-31). Katika maandishi ya wanahistoria wengine haiko hivyo na
kutoka katika maandiko ya kale tunajua kuwa Nabonidus ndiye alikuwa
mfalme wa mwisho wa Babeli kabla ya uvamizi wa Wamedi na Waajemi
uliopelekea mwisho wa dola ya Wakaldayo. Kama Daniel alikuwepo enzi
hizo aliwezaje kukosea kitu kilicho wazi hivi? Na kama alikosea jambo
rahisi kama hili tutaaminije kama kitabu hiki sio utunzi wa Mtu
fulani baada ya matukio (ambapo ni rahisi kukosea kwa kuwa hakuwepo)?
Jibu
Danieli ni moja ya vitabu vya Biblia
ambavyo vimeshambuliwa sana, na kwa sababu ambayo mtu yeyote
aliyeyasoma haya au kuyatafiti atayaelewa. Wenye kushuku na
wasioamini Biblia hawana jinsi ya kutimiza malengo yao bila
kushambulia vitabu hivi kwa kuwa vimejaa uthibitisho kuwa Biblia
haiwezi kuwa Neno la mwanadamu kwa kuwa imetabiri kwa kina matukio,
na mambo na falme kwa usahihi kiasi kwamba hakuna namna mwanadamu
angeweza kuandika. Moja ya vitabu vya Biblia vyenye unabii huu wa
kutisha ni kitabu cha Daniel.
Mashambulizi hayakuanza jana wala juzi.
Polfili, mwanafalsafa wa kipagani ni moja kati ya watu wa mwanzo
kabisa kukishambulia kitabu hiki. Hatujabakiwa na kazi zake ila
tunaweza kujua kupitia wanatheolojia waliokuwa wakijibu mashambulizi
haya. Mathalani, Jerome katika maoni yake juu ya kitabu cha Danieli
anasema
“Polfili aliandika katika kitabu
chake cha kumi na mbili dhidi ya unabii wa Danieli, akikana kwamba
kiliandikwa na mtu ambaye kitabu hiki kimepewa jina lake, ila mtu
mwingine aliyeishi Yudea wakati wa Antiokasi aliyeitwa Epifania. Na
zaidi ya hayo anadai kuwa “Danieli” hakutoa unabii juu ya wakati
ujao kama ambavyo alisema juu ya wakati uliopita, na mwisho kuwa
chochote alichosema mpaka wakati wa Antiokasi kilikuwa ni historia
thabiti, wakati chochote alichojaribu kubahatisha zaidi ya wakati ule
kilikuwa si kweli, kama ambavyo asingeweza kujua wakati ujao”
Mashambulizi ya leo juu
ya kitabu hiki aidha ni marudio ya mwanafalsafa huyu, yakiwa
yamepakwa rangi ya ukisasa au ni mapya yakifuata msingi wa Polfili.
Kitu kimoja ambacho kilimfanya huyu mwanafalsafa afikie hitimisho
lake hili ni kuwa maandiko katika Danieli yalitimia hata nukta. Kwa
akili timamu ya kawaida kabisa, hakuna namna Danieli angeweza kujua
mambo yajayo kwa usahihi hivyo: alijua haukuwa ubahatishaji. Kwa hiyo
alibakiwa na njia mbili za kufuata. Aidha Daniel aliandika karne ya 6
K.K au atengeneze namna ya maelezo kuwa ni uhuni uliofanywa baada ya
matukio. Bahati mbaya alichagua njia ya pili ambayo siyo ya kweli.
Nikirudi kwenye swali la
leo ambalo wengi wa wanaolitumia kama ngao ya kukwepa kuiamini Biblia
hufuata nyayo za Polfili, limetokana na kutokuelewa historia na
kutojishughulisha. Japo wengi wamelikimbia swali hili na hawalitumii
tena, bado wapo wenye kushuku wanaolitumia ili pengine kuwapotosha
Wakristo wachanga na wengine wasiojua. Mfano katika maandiko yao,
“Skeptic Annotated Bible” wameandika “mfalme wa mwisho wa
Babeli alikuwa Nabonidasi aliyetawala toka 556 mpaka 539 and
aliyeshindwa na Koreshi. Alikuwa Nabonidasi na si Belshaza aliyekuwa wa mwisho katika wafalme wa Babeli.”
Kwanza
hatutumii historia kujaribu kuhukumu Neno la Mungu. Wanahistoria nje
ya Biblia wamekuwa wakikosea mambo mengi na hata majina mbalimbali,
na unapofanyika ugunduzi wa mambo ya kale, Biblia imekuwa
ikithibitishwa kuwa sahihi. Hata hivyo, kwa hili historia ya nje ya
Biblia iko sahihi, na Biblia haijakosea. Mfalme wa mwisho wa Babeli
hakuwa Belshaza bali Nabodinasi. Na ndio maana Biblia inasema
yafuatayo baada ya Danieli kutafsiri maneno yaliyoandikwa na kiganja
mbele ya Belshaza:
Ndipo
Belshaza akatoa amri, nao wakamvika Danieli mavazi ya rangi ya
zambarau, wakatia mkufu wa dhahabu shingoni mwake, wakapiga mbiu
kutangaza habari zake, ya kwamba yeye ni mtu wa tatu
katika ufalme. (Danieli 5:29)
Hapa
Daniel anapaswa kuwa mtu wa tatu kwa kuwa tayari Belshaza alikuwa ni
mtu wa pili na kwa hiyo alikuwepo mtu wa kwanza, naam, naye ni mfalme
Nabodinasi. Katika andiko la
Nabonidus mwenyewe linalofahamika kama "Nyakati za Nabodinasi"[1]
tunajua kuwa "Mfalme alitumia miaka kumi huko Araba na akaacha
Babeli ikisimamiwa na mwana wake Bel-Shar-Usur [Belshaza]".
Kwa hiyo wakati nabonidasi hakuwepo Mfalme wa Babeli alikuwa Belshaza
lakini akiwa mtu wa pili na si wa kwanza. Kwa hiyo Biblia hapa ipo
sahihi kwa kuwa Danieli, aliyeandika kitabu hiki alishuhudia
aliyoyaona.
Kuna Jambo kubwa zaidi ya
hili la Danieli kuwa sahihi. Nalo ni kuwa Mungu aliyesema na Danieli,
Yeye aliyeumba mbingu na nchi, ametenga siku awahukumu wanadamu wote
sawasawa na matendo yao. Mungu atatuhukumu si kwa matendo tu yaliyo
maovu bali hata mawazo na nia ovu zote. Siku hii ya kutisha inakuja
na njia pekee ya kuepuka hukumu hii ni kujisalimisha kwa Yesu Kristo,
yeye aliye mwokozi wa wanadamu wote. Leo hii umlilie yeye, utubu na
kugeuka toka njia zako mbaya. Naye atakusamehe makosa yako na kukupa
uzima wa milele. Kumbuka Yesu anakuja, furaha kwa watu wake na
huzuni, kilio na kusaga meno kwa waliomkataa.
Maranatha!
[1] http://www.britishmuseum.org/explore/highlights/highlight_objects/me/c/cuneiform_fall_of_a_dynasty.aspx
No comments:
Post a Comment